Baada ya kusambaa kwa taarifa mitandaoni zinazodai kwamba aliyekuwa mgombea urais wa Chama cha ACT-Wazalendo Bernard Membe, kuwa atajitoa katika chama hicho Januari mosi mwakani, uongozi wa chama hicho umesema haupo tayari kuzungumzia suala hilo kwa sasa.
Akizunguza na EA Digital Katibu Mkuu wa chama hicho, Ado Shaibu, amesema hawapo tayari kuzungumzia suala hilo kwani kwa sasa wana mambo ya kuwaelekeza Watanzania baada ya Kikao cha Kamati Kuu kumalizika jana Desemba 5, 2020.
“Watanzania wanahitaji kufahamu Kamati Kuu imeamua nini kuhusu masuala yaliyopo mbele yetu ambayo tulijadili na tutatoa taarifa hapo baadaye na sio masuala ya Bernard Membe, sio muda wake kwa sasa nitafutwe wakati mwingine,”amesema Ado.
Membe aliyewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje ni mwanachama mwenye kadi namba 2 na Mshauri Mkuu wa chama hicho alijiunga na ACT- Wazalendo Julai 16, 2020 na aligombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia chama hicho akaibuka na kura 81,129 sawa na asilimia 0.5% ya kura zote.
Membe kada wa muda mrefu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) alijiunga chama cha ACT-Wazalendo mwaka huu baada ya Februari 28, 2020 kufukuzwa uanachama wa CCM na Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM.