Hatimaye mchekeshaji @ericomond amejipatia jiko, mrembo anaefahamika kwa jina la Carol, kupitia ‘The Wife Material Show’ kipindi alichokianzisha mchekeshaji huyo kutoka Kenya kwa lengo kuu la kumsaidia kupata mke wa kuoa na mama wa watoto wake, huku akitoa ahadi ya kufunga ndoa na msichana atakaeibuka mshindi kwenye show yake hiyo.


Taarifa hizo njema zinaambatana na taarifa ambazo si nzuri kidogo kwa #EricOmondi, baada ya staa huyo kujikuta kwenye rada za mkurugenzi wa bodi ya uainishaji wa filamu nchini Kenya (KFCB) Dr. Ezekiel Mutua, akimshutumu kwa kuwadhalilisha wasichana wa Kenya kingono, kwa mwamvuli wa sanaa.


“Kwanza kuna Corona, lakini huyu ‘mpuuzi’ amekuwa akiwabusu wasichana kadhaa na kuwarekodi video kwa jina la sanaa” aliandika Dr. Mutua kwenye ukurasa wake wa Facebook.


Aliendelea kuelezea kuwa hata studio za #Omondi alizozifungua, hazina lengo la kukuza sanaa badala yake ni sehemu ya kuwanyanyasa wasichana kingono.


“Ofisi alizozifungua huko Lavington kama studio, si lolote zaidi ya ‘danguro’ tu, ni sehemu ambayo wasichana wadogo wanadhalilishwa kingono kwa jina la sanaa, kitendo cha taasisi na makundi ya haki za wanawake kukaa kimya wakati hili likitokea na polisi kutokuwakamata waliohusika na maovu haya, ni ushahidi tosha kuwa sisi kama jamii tumekuwa wa ovyo kabisa”


Dr. Mutua alienda mbali zaidi na kuwaomba polisi wa nchini Kenya kuwakamata wafanyakazi wa studio za Eric Omondi, zilizoko huko Lavington, Nairobi.


Wiki kadhaa zilizopita, #EricOmondi alitumia ukurasa wake wa Instagram kuanzisha kipindi chake hicho cha ‘Wife material Show’ kwa nia ya kupata mke, na alifikia hatua hiyo baada ya kudai kuwa wanawake wengi aliokuwa akiwafungukia kuwa anataka kuwaoa walikuwa wakichukulia kama ni sehemu ya vichekesho vyake.