liyewahi kuwa mbunge wa jimbo la Singida Mashariki kupitia CHADEMA Tundu Lissu, Julai 27, 2020, alikanyaga ardhi ya Tanzania kwa mara ya kwanza tangu alipoondoka nchini baada ya kushambuliwa kwa risasi na watu wasiojulikana nyumbani kwake Dodoma, wakati akitoka kuhudhuria vikao vya Bunge.



Tundu Lissu, Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA na aliyekuwa mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 28, 2020.


Lissu aliwasili katika uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Jijini Dar es salaam, siku ya Jumatatu mchana akitokea Brussels, Ubelgiji, alikokuwa akifanyiwa matibabu, baada ya kushambuliwa mwaka 2017.


Maelfu ya wananchi wengi wakiwa wamevalia nguo zenye rangi ya chama chake na wengine wakipeperusha bendera ya chama hicho walijitokeza katika uwanja huo kumlaki, wakiongozwa na viongozi wakuu wa chama hicho Freeman Mbowe pamoja na John Mnyika.


Katika hotuba zake mara baada ya kuwasili nchini, Lissu alitoa pole kwa Watanzania kufuatia kifo cha aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tatu, Mzee Benjamin William Mkapa, ambaye alifariki dunia usiku wa kuamkia Julai 24, 2020.


Mbali na pole hizo Lissu pia alielezea mateso aliyoyapata mara baada ya shambulizi lile, huku akidai kuwa alitamani kuibusu kwa mara ya kwanza ardhi ya nchi yake lakini alishindwa kwa kuwa goti lake moja hawezi kulikunja kutoka na athari ya risasi alizoshambuliwa nazo, pia aliwashukuru Watanzania wote na wasio Watanzania waliojitolea kumuombea na kumpatia damu wakati alipokuwa hajiwezi.


Mbali na tukio la Lissu kuwasili nchini, pia alishiriki katika kinyang'anyiro cha Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 28, 2020, akipeperusha bendera ya kiti cha urais kupitia chama hicho, ambapo katika kampeni zake aliahidi mambo kedekede na alibahatika kuzunguka katika maeneo mbalimbali ya nchi na kufanya kampeni zake.


Baada ya mchakato mzima wa zoezi la uchaguzi mkuu, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), ilimtangaza mshindi wa kiti cha urais kuwa ni Dkt. John Pombe Magufuli, wa CCM aliyepata kura milioni 12.5 sawa na asilimia 84, huku Lissu yeye akipata kura milioni 1.9.


Mara baada ya mchakato wa uchaguzi kukamilika, mshindi kutangazwa na Rais Dkt. Magufuli, kula kiapo cha kuendelea kuiongoza Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mara ya pili, mnamo Novemba 10, 2020, Lissu aliondoka nchini kurejea nchini Ubelgiji, huku akidai kuwa haondoki nchini kama mkimbizi wa kisiasa bali anakwenda huko kujipanga zaidi kisiasa. Aidha Lissu pia bado anaendelea na matibabu yake.