Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Innocent Bashungwa amesema Taifa limepata pigo kwa kuondokewa na Mtendaji wake mchapakazi, Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) Godfrey Mngereza.

Waziri Bashungwa ameyasema hayo jijini Dar es salaam wakati wa shughuli ya kuaga mwili wa Mngereza katika viwanja vya Karimjee.

Amesema katika uhai wake Mngereza alisimamia Tasnia ya Sanaa na kuleta mabadiliko miongoni mwa Wasanii ambao wengi wao walifanya kazi zao kwa kuzingatia mila na desturi za Mtanzania.

Kwa mujibu wa Waziri Bashungwa, Serikali itaendeleza mambo mazuri aliyoyaacha Marehemu Mngereza, yaliyokuwa na lengo la kuleta mabadiliko kwa Wasanii na kazi zao.

Awali akimkaribisha Waziri Bashungwa, Msemaji Mkuu wa Serikali na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt Hassan Abbasi amewataka Wasanii nchini na Watanzania wote kumuenzi kwa vitendo Marehemu Mngereza aliyejitolea na kuipenda kazi yake hadi umauti  unamkuta.

Miongoni mwa Viongozi waliohudhuria shughuli hiyo ya kumuaga Marehemu Mngereza katika viwanja vya Karimjee ni Naibu Waziri Wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Abdallah Ulega, Katibu wa NEC Itikadi na Uenezi Humphrey Polepole na Mkuu wa mkoa wa Dar es salaam Aboubakar Kunenge.

Mwili wa Mngereza unasafirishwa mchana huu kuelekea Suji, Same mkoani Kilimanjaro kwa ajili ya.mazishi yatakayofanyika kesho.

Mngereza ameacha Mke na Watoto Watatu, ,Bwana ametoa, Bwana ametwaa jina lake lihimidiwe Amen.