JAMBO limezua jambo! Kitendo cha staa wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ au Mondi kumtakia heri ya siku ya kuzalia mwanaye Nillan kimemgeukia mkali huyo, wananzengo wamemuibulia mazito, AMANI linakushia habari hii ya motomoto.


Ishu hiyo imeibuka mapema wiki hii wakati Nillan anayeishi Sauz na mama yake Zarinah Hassan ‘Zari The Boss Lady’, alipokuwa akisherehekea siku yake ya kuzaliwa na Mondi kuandika ujumbe huu kwenye ukurasa wake wa Instagram: “4 Years ago God Blessed me with a Cute Baby Boy, and we Called him NILLAN, @princenillan ….and today we are celebrating his Reborn…


Happy Birthday my Beloved Son, Mwenyezi Mungu akupe akili na maarifa kama za baba na mama yako ili uje kuviendeleza vidogo tulovianzisha na kuzidi kutengeneza fursa kwa Waswahili wenzetu.”


MAMBO YAIBULIWA

Baada ya kuandika ujumbe huo, wananzengo waliibuka kama wote na kuanza kumkosoa Mondi kwa kitendo cha kumuandika Nillan kama mrithi wa mali zake wakihoji kuhusu watoto wengine ambao Mondi amezaa na wanawake tofauti; Dayllan na Naseeb Junior.


“Haiwezekani aseme aje kuviendeleza kwani watoto wengine hawataviendeleza? Huu ni ubaguzi wa watoto ambao mara kwa mara Mondi amekuwa akiufanya.”


“Huyu Mondi hana maana kabisa, kwa nini siku zote anapozungumzia watoto anawapa sana kipaumbele watoto aliozaa na Zari sijui kwa nini mimi ananiudhi sana, huu ni ubaguzi na haukubaliki.” “Kwani kuna sababu gani kusema atakuja kuendeleza?


Watoto wengine watajisikiaje? Mama zao je anadhani watajisikiaje, huyu dogo tatizo lake hajielewi. Busara hana kabisa.” Hayo yalikuwa ni baadhi ya maoni ambayo yalichangiwa na watu mbalimbali kwenye mtandao huo wa kijamii wa Instagram.


MONDI KIMYA

Hata hivyo pamoja na kuandamwa na maoni hayo na mengine makali ambayo yalikuwa mengine yakimtusi, Mondi aliamua kukaa kimya na hakuonekana kujibu lolote kwenye posti yake hiyo.


WENGINE WAFUKUA MAKABURI

Kuna baadhi walienda mbali na kuanza kufukua makaburi ya habari ambayo iliwahi kuandikwa na gazeti dada na hili la IJUMAA WIKIENDA iliyokuwa na kichwa cha habari kilichosomeka; MONDI AWANYIMA URITHI WANAWE.


“Huyu nahisi atakuwa tu anajisafisha kwa kujifanya anampa urithi Nillan wakati alishasema kwamba hawa bado ni wadogo na vitu vingi amemweka mama yake kama mrithi,” aliibua mjadala mpya. Kitendo cha jamaa huyo kuibua mada hiyo, kilizidi kuchochea moto wa watu kumuandama Mondi kupitia mtandao huo wa Instagram.


MSINGI WA HABARI HIYO…

Kwenye habari hiyo ya IJUMAA WIKIENDA, Mondi alidaiwa kumuandika mama yake kwenye mali zake nyingi ikiwemo hoteli aliyoinunua maeneo ya Mikocheni, nyumba, magari pamoja na vituo vyake vya habari.


Kuonesha kuwa ni kweli Mondi humuandika mama yake kwenye mali zake, gazeti hilo lilinukuu moja ya maelezo yake aliyoeleza kuhusu urithi wa mali zake: “Mimi si mtu wa kujikweza kuonesha kwamba hii hoteli itakuwa ni ya Tiffah au Wasafi FM ni ya Nillan au Wasafi TV ni ya Dyllan.


“Watoto wangu bado ni wadogo sana, natamani wangekuwa wakubwa ili waweze kusimamia miradi yangu,” anukuliwa Mondi na gazeti hilo.


TUJIKUMBUSHE

Mondi amezaa watoto wanne na wanawake watatu tofauti ambao ni Zarinah Hassan ‘Zari The Boss Lady’ ambaye amezaa naye watoto wawili, Latiffah Nasibu ‘Tiffah Dangote’ na Prince Nillan. Wengine ni mwanamitindo Hamisa Mobeto ambaye amezaa naye mtoto mmoja, Dyllan na Tanasha Donna ambaye amezaa naye mtoto mmoja aitwaye Naseeb Junior.