Kundi la Watalii 37 kutoka nchini Japan liliwasili nchini kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) kwa ajili ya kutalii sambamba na kufanya mikutano ya mafunzo.
Watalii hawa wanaofahamika kama Klabu ya Mabilionea (Billionaires Club) watakuwepo nchini kuanzia tarehe 3 hadi 10 Disemba 2020. Watalii hawa ambao watatembelea vituo mbalimbali vya utalii nchini ni viongozi na wamiliki wa makampuni kutoka katika sekta mbalimbali nchini Japan.
Watalii hao mara baada ya kuwasili nchini walipata fursa ya kusikiliza mawasilisho (presentation) kutoka taasisi mbalimbali kama vile Mamlaka ya Hifadhi Tanzania, Kituo cha Uwekezaji Tanzani na Bodi ya Utalii ya Tanzania ambapo, sambamba kufahamishwa zaidi kuhusu Tanzania, vilevile walielezwa kuhusu fursa na taratibu za kuwekeza katika sekta mbalimbali nchini.
Watalii hao wengi walionesha kuvutiwa na fursa za uwekezaji zilizopo nchini na kuridhishwa na namna Serikali ilivyoandaa mazingira rafiki kwa wawekezaji.
Akizungumza baada ya kusikiliza mawasilisho Bi. Nanako Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya kutengeneza viungo bandia vya binadamu, alisema amevutiwa na fursa zilizopo katika sekta ya afya na namna Serikali ilivyojiandaa kutoa motisha kwa wawekezaji wa eneo hilo hapa nchini. Maeneo mengine ya uwekezaji yaliyowavutia watalii hao ni sekta ya utalii, usafirishaji, kilimo na viwanda.
Watalii hawa wametembelea hapa nchini kwa juhudi kubwa za utangazaji na uhamasishaji utalii zinazoendelea kufanywa na Bodi ya Utalii Tanzania kwa kushirikiana na Ubalozi wa Tanzania nchini Japan ambao unafanya juhudi kubwa ya kufungua soko la utalii la Japan kwa vivutio vya utalii vinavyopatikana hapa nchini hasa baada ya mlipuko wa ugonjwa wa Corona.
Vilevile watalii hao wametaja mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Tano ikiongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli katika kupambana na mlipiko wa ugonjwa wa CORONA, amani iliyopo nchini, ukarimu wa watanzania na uwepo wa vivutio hadhimu vya utalii nchini ni miongoni mwa sababu nyingi zilizowafanya kuja kutalii Tanzania.
Akizungumza wakati wa mapokezi ya Watali hao Mwenyekiti wa Bodi ya Utalii Tanzania Haji Thomas Mihayo alisema Ilani ya chama cha mapinduzi ya mwaka 2020-2025 inazungumzia kukuza utalii wa mikutano ili kuongeza idadi ya watalii wanaotembelea hapa nchini Pamoja na kuongeza mapato kufikia Dola Billioni 9.
“Sisi Bodi ya Utalii Tanzania Pamoja na Balozi zetu utekelezaji wa ilani umeshaanza mara moja, kwani katika kipindi hiki cha miaka mitano ya pili ya awamu hii ya tano ya muheshimiwa Rais Dr. John Pombe Magufuli tunalengo la kufikia watalii million 5 na utalii wa mikutano ni moja ya aina za utalii zitakazosaidia kufikia lengo hilo.