MASTAA wengi wamekuwa na tabia ya kuwaficha wazazi wao, ikiwa kuna sababu kama kuu mbili, ambapo ya kwanza ni kwa sababu wengi wao hawapendi kuwashirikisha wazazi wao kwenye mitandao ya kijamii na ya pili kutokana na hali mbaya au duni walizonazo wazazi wao, lakini kwa upande wa msanii wa kizazi kipya Lulu Abbas ‘Lulu Diva’ ambaye mama yake ni mgonjwa takriban miaka sita, amesema kuwa kamwe hawezi kumficha mama yake.

 

Msanii huyu wa Bongo Fleva ambaye hivi karibuni aliachia video kali ya wimbo wake wa ‘Hauna Maajabu’ amesema kuwa aliamua kumuonyesha mama yake kwenye mtandao wa kijamii wa Instagram hivi karibuni baada ya kutofanya hivyo kwa muda mrefu.

 

Pamoja na jambo hilo, Amani Showbiz Extra imefanya mahojiano marefu na mrembo huyo kama ifutavyo:

Amani: Hongera Lulu, kwa video kali ya Hauna Maajabu.

Lulu Diva: Asante sana, ni kweli kabisa ya duniani hakuna maajabu kabisa.

 

Amani: Siku za hivi karibuni nimeona wazi unapiga sana hatua kwenye muziki wako, nani anakusukuma zaidi?

Lulu Diva: Hakuna anayenisukuma zaidi bali ni mimi mwenyewe kwa sababu hata kuamua kuimba ni jitihada zangu mwenyewe na si mtu mwingine, hivyo mpaka hapa nilipo kwa kweli niliamua kujifunga mkanda mpaka nikatimiza lengo langu.

 

Amani: Lakini najua huko nyuma ulikuwa kwenye ugizaji na uliweza kufanya filamu zaidi ya mbili, bado unaweza kuigiza kwa sasa?

Lulu Diva: Ni kweli nilianza kwenye kuigiza, lakini kwa sasa siwezi tena kwa sababu nimejikita sana kwenye kuimba, na hapa nawaza kila siku wimbo gani, mzuri watu waupende na ubambe.

 

Amani: Huko nyuma kidogo, kulikuwa na tetesi za kutoka na kigogo ambaye alikupangishia nyumba ya kifahari na kukununulia vitu thamani, vipi mliachana?

Lulu Diva: Yaani hayo mambo ya zamani sana hata huyo mtu nilishamsahau kabisa, maana niliendelea na mambo mengine na hata ukiniuliza yuko wapi sijui.

 

Amani: Kwa nini mliachana?

Lulu Diva: Alijua nina mahusiano mengine kwa hiyo tukawa na ugomvi mkubwa sana.

Amani: Sasa kwa nini uwe kwenye mahusiano na mtu mwingine na tayari upo naye?

Lulu Diva: Sasa yeye alikuwa ni mume wa mtu sasa hata kama ningeendelea naye huko mbele ingekuwaje?

 

Amani: Lakini pia hapa kati tulisikia kuwa mwanaume ambaye alikupa gari aina ya Jeep, alikuwa anakufanyia sana fujo umrudishie gari lake, hiyo ikoje?

Lulu Diva: Ni kweli lakini umeona wapi mtu unampa gari mpenzi wako halafu mkiachana analichukua, mimi nimekomaa tu, na mara nyingi alikuwa ananifanyia fujo nyumbani kwangu ila sasa hivi kapumzika kidogo.

Amani: Tetesi za kuzaa mtoto na kumtelekeza kijijini bado zinakutafuna, sasa kama sio kweli kwa nini watu bado wanaendelea kusema hilo?

 

Lulu Diva: Hivi kweli sasa hivi kuna hayo mambo kweli, yaani uzae mtoto kabisa kisha umtelekeze kisa nini, na hata kama itakuwa hivyo basi angekuwa hapa maana mama yangu mzazi nakaa naye sasa huko kijijini ningemuacha atakaa na nani.

Amani: Hivi karibuni niliona umeanza kumuonyesha mama kwenye mtandao wako wa kijamii wa Instagram, na watu waakaanza kusema kuwa kwa nini unamuonyesha mama mgonjwa, hii vipi?

 

Lulu Diva: Hivi unajua binadamu hawana wema kabisa, nilivyokuwa simuonyeshi walisema nimemtelekeza mama yangu, lakini nilivyomuonyesha shida, ni hivi mama yangu simnadi na siwezi kufanya hivyo, yule ni Mungu wangu wa pili, siwezi kumficha hata kidogo na wala sitarajii hivyo, najua anaumwa hawezi kutembea lakini nafanya niwezavyo ili mama yangu awe na furaha tu.

 

Amani: Kwa hiyo sasa hivi unakaa naye?

Lulu Diva: Ndio niliona ni vyema niwe namuona kuliko kuwa naye mbali maana zamani alikuwa akikaa Tanga.

Amani: Haya shukrani.

Lulu Diva: Asante sana.