Mshambuliaji wa klabu ya Liverpool, Sadio Mane alitumia mchezo wa jana dhidi ya Ajax wa ligi ya mabingwa Ulaya, kutoa heshima kwa Papa Bouba Diop aliyefariki wiki iliyopita.

 

Mane ambaye ndiye nahodha wa Senegal, aliisaidia Liverpool jana kushinda bao 1-0, alivua jezi na kubakia na fulana ya ndani iliyoandikwa PAPA BOUBA DIOP ikimaanisha kumbukumbu  juu ya gwiji huyo aliyewasaidia Simba wa Teranga kufanya vyema katika michuano ya kombe la Dunia mwaka 2002.


Bao la Liverpool lilifungwa na Curtis Jones dakika ya 58 na kuwafanya majogoo hao kufikisha alama 12 na kuziacha Atalanta ambao walitoka sare ya bao 1-1 na Midtylland kuwa na alama 8 wakati Ajax wana alama 7 .


Matokeo mengine katika michezo ya jana, Fc Porto ilitinga hatua ya 16 bora baada ya kupata suluhu na Manchester City, na sasa wamefikisha alama 10 huku City wakiwa na alama 13, na kuziacha Olimpiacos na Marseille wakibakia na alama tatu.


Atletico Madrid walitoka sare ya bao 1-1 na mabingwa watetezi Bayern Munich, nayo RB Salzburg iliitandika Locomotive Mosco bao 3-1, Real Madrid ilikubali kisago cha bao 2-0 kutoka kwa Shaktar Donestk ,nayo Inter Milan ikaibamiza Borussia Monchegladbach bao 3-2.