UNAPOTAJA jina la mwanamuziki mkubwa barani Afrika, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ kutoka Tanzania, akili za wengi zinakimbilia kwenye kufuru zake za pesa.


AYAWEKA MAISHA HATARINI


Habari mbaya kwake ni kwamba, kufuru hizo sasa zimemfanya kuyaweka maisha yake hatarini kiusalama kwani anaweza kuvamiwa muda wowote na majambazi wakizihitaji pesa hizo.


Diamond au Mondi amekuwa siyo msiri linapokuja suala la pesa nyingi anazopiga kupitia vitega-uchumi vyake ambapo amekuwa akijitangaza bila kujua madhara yake.


ANAWARINGISHIA WATU?


Kupitia ukurasa wake wa Instagram katika kipengele cha Insta Story, Mondi amekuwa akiweka clips (vipande vifupi vya video), ama akipanga maburungutu ya pesa kabatini au benki au akizihesabu na kuonekana kama anawaringishia watu.


Katika moja ya video hizo, Mondi anaonekana akiwa amepanga maburungutu ya noti za shilingi elfu kumikumi na Dola za Kimarekani kwenye ambazo siyo rahisi kuzihesabu kutokana na wingi wake.


MONDI ANAWAKERA


Hata hivyo, kwa upande wake, Mondi amekuwa akijitetea kuwa anafanya hivyo kama sehemu ya hamasa kwa vijana wengine kuwa na hasira ya kutafuta pesa.


“Ninakukera ili upate hasira za kutafuta pesa…” Anasikika Mondi kwenye moja ya video hizo na kuongeza;


“Mimi ndiye msanii tajiri zaidi…”


Jambo hilo limeendelea kuzua mjadala mzito kwenye mitandao ya kijamii ambapo ‘chawa’ wa Mondi wamekuwa wakishangilia na kuwataka anaowakera nao kutafuta pesa kama Mondi.


 


“Watasonya na kununa, fanyeni kazi vijana, chuki ni maradhi ya kifo, mtakufa,” anasema Juma Lokole juu ya mjadala huo na kusababisha wengine kutiririka;


“Staa na tajiri alikuwa ni mmoja tu…Ginimbi (marehemu)


“Mwambieni Mondi anajihatarishia maisha. Kuna watu hawajashika buku kumi tangu mwaka huu umeanza. Shauri yake…


 


“Wabongo tumejawa na chuki sana, pesa siyo majani, mwambieni Simba (Mondi) kuna leo na kesho…


“Diamond kufanya hivyo ni ushamba na akiambiwa ni mshamba anakasirika…


“Ni ushamba wa hali ya juu sana, kuna matajiri wana pesa kuliko yeye, lakini hawawezi kufanya hivyo…Kuna Bill Gates, kuna Aliko Dangote…huwezi kukuta wameweka mambo kama hayo…


 


“Wenye chuki tafuteni pesa acheni kumezea mate pesa za wengine.


“Kwani hajui benki? Kwa nini anakaa na penzi nyingi hivyo? Huku ni kujihatarishia maisha…” Ilisomeka sehemu ya maoni mengi juu ya mjadala huo huku wakiuomba uongozi wake kumuongezea ulinzi.


 


MAJIRANI NAO


Gazeti hili lilifika nyumbani kwa Mondi maeneo ya Mbezi-Beach jijini Dar na kukuta ulinzi wa kutosha nyumbani kwake.


 


Hata hivyo, baadhi ya majirani walilieleza gazeti hili kuwa, pamoja na kwamba ana ulinzi wa kampuni binafsi wa askari wanne wenye silaha, lakini bado kuna watu wengi wanafika mahali hapo kutaka misaada mbalimbali ya kipesa kutokana na kumuona akifanya kufuru za pesa mitandaoni.


Hata hivyo, walitahadharisha uongozi wake kuchukua hatua kwani anayaweka hatarini maisha yake.




WAKUBWA WAMUONYA


Taarifa za ndani zimeeleza kuwa, mara baada ya kuwa anafanya hivyo, wapo baadhi ya viongozi Serikalini na wanasiasa wenye ukaribu na Mondi ambao wamekuwa wakimwambia asiwe anafanya hivyo kwani ataonekana kama anawaringishia wengine.


 


Inaelezwa kuwa, wakubwa hao wamekuwa wakimweleza kuwa, anapofanya hivyo, wapo watakaotafuta namna ya kuzichukua kwa njia za kihalifu.




HUWEZI KUMFIKIA MONDI KIRAHISI


Gazeti hili lilimtafuta mmoja wa mameneja wa Mondi, Said Fella ‘Mkubwa’ ambaye alisema kwa sasa jamaa huyo ana ulinzi mkubwa na kwamba, si rahisi kwa mtu kumfikia na kumdhuru.


 


“Huwezi kumfikia kirahisi. Utakutana na ulinzi mzito wa askari wa getini, utakutana na ulinzi binafsi wa mabodigadi wake ambao wanatembea naye kila anapokuwa na mizunguko.


“Kwenye shoo, akiwa kwenye mizunguko yake binafsi na popote ulinzi upo wa kutosha,” anasema Fella.


 


SI MONDI PEKEE


Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kwamba, si Mondi pekee mwenye tabia hiyo ya kucheza na maburungutu ya pesa.


Wengine wenye rekodi hiyo ni pamoja na Faustina Charles ‘Nandy’ na mpenzi wake, William Lymo ‘Billnass’ na wengine wengi.


STORI: KHADIJA BAKARI