MWENYEKITI wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba na mwekezaji wa timu hiyo, Mohamed Dewji ‘Mo’, amesema licha ya timu yake kufanikiwa kutinga hatua ya awali wa Ligi ya Mabingwa Afrika, hajafurahishwa na ubutu wa safu ya ushambuliaji na kusema kocha Sven Vandenbroeck anahitaji kufanyia kazi.

 

Mo alisema jambo kubwa lilikuwa ni kupata nafasi ya kufuzu hatua inayofuata na hilo lilifanikiwa, ingawa bado kuna tatizo kwa washambuliaji kushindwa kufunga mabao ya kutosha na kuongeza kuwa bao moja walilopata ugenini ndilo ambalo liliwabeba.

 

Simba walitoka suluhu na Plateau United, Jumamosi katika Uwanja wa Benjamin Mkapa na kufanikiwa kusonga mbele kwenye hatua inayofuata kwa faida ya bao la ugenini walilopata kwenye mchezo wa kwanza uliopigwa nchini Nigeria wiki iliyopita.

 

Akizungumzia uhaba wa mabao kwenye mechi hizo mbili za kimataifa, Mo alisema: “Kiukweli nashukuru kwanza kwa kuwa tumefanikiwa kufuzu hatua inayofuata, ila ukweli ni kwamba sijafurahishwa na eneo la ushambuliaji kwa kushindwa kufunga mabao ya kutosha, nafi kiri mwalimu na benchi la ufundi wanatakiwa kulifanyia kazi hilo.

 

“Kama tusingepata bao kule ugenini, basi huenda hali ingekuwa mbaya kwetu. Kuna haja ya kufanyia kazi upungufu huo mapema kwani tunakokwenda ni pagumu zaidi,” alisema Mo.

 

Safu ya ushambuliaji ya Simba iliyocheza dhidi ya Plateau ni John Bocco na Meddie Kagere ambaye juzi alicheza dakika mbili tu baada ya kuingia dakika ya 90 na mashabiki kulalamika kwa nini aliachwa nje ya uwanja kwa muda mrefu kiasi hicho.

GPL