Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad ameahidi kuwatumikia Wananchi wa Zanzibar akiwa katika wadhifa huo.

Akizungumza mara baada ya kuapishwa kushika rasmi wadhifa huo Ikulu jijini Zanzibar, Maalim Seif amewashukuru Wananchi wa Zanzibar kwa imani kubwa walioionesha kwake.

Maalim Seif ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama Cha ACT Wazalendo, amekishukuru chama chake kwa kumpendekeza kuwa Makamu wa Rais wa Zanzibar.

Amesema uamuzi wa Chama Cha ACT Wazalendo kuingia katika serikali ya Umoja wa Kitaifa haukuwa rahisi, lakini waliamua kuuridhia kutokana na dhamira ya dhati ya Rais wa Zanzibar Dkt Hussein Mwinyi ya kushirikian na chama hicho.

Amewataka Wananchi wote wa Zanzibar wa ndani na nje, kushirikiana ili kuijenga Zanzibar na ameahidi kushirikiana na Rais Mwinyi.

Disemba 6 mwaka huu Rais Mwinyi alimteua Maalim Seif Sharif Hamad kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar.