STAA mkali wa filamu, Kajala Masanja amevunja ukimya kwa kukanusha madai mazito ya kutoka kimpenzi na msanii wa Bongo Fleva, Rajabu Abdukahari ‘Harmonize’ ambaye pia ni mmiliki wa Konde Gang.

Akizungumza na RISASI JUMAMOSI, Kajala alisema siku zote jambo usilolijua ni sawa na usiku wa giza.

 

Alisema watu wengi wasiokuwa na kazi ya kuwaingizia kipato, huwa bize na mitandao ya kijamii na kuanza kuwatungia watu mambo yanayoweza kuwaharibia maisha yao.



“Mitandao siku hizi inatumika vibaya, inatumika kuharibu maisha ya watu… wapo wanaoitumia kuwatungia watu uongo.“Kuna mtu kashupalia kuwa ninatoka kimpenzi na Harmonize hadi ananiudhi sana, maana utadhani anao ushahidi mkononi,” alisema.

 

Alisema watu hao wanaomzushia kutoka na Harmonize, watambue kuwa na yeye ana mahusiano yake na mtu mwingine na si Harmonize.“

 

Hebu wafikirie huyu mtu wangu akisikia hivyo itakuwaje, hata kama hatayazingatia haya mambo ya mitandaoni lakini moyoni mwake huwezi kujua anawaza nini, vivyo hivyo kwa Harmo na huyo mpenzi wake.“

 

Naomba watu watambue kuwa kila mmoja wetu yupo kwenye mahusiano yake ya kimapenzi… sasa kuendelea kutuzushia kuwa tunatoka pamoja huko ni kuharibiana maisha kitu ambacho sio kitu kizuri kabisa. Waache kuharibu mahusiano ya watu,” alisema Kajala.



Staa huyo aliongeza kuwa kama uhusiano na msanii huyo ungekuwepo basi kipindi cha nyuma wasingepelekana polisi.“Watu hata kujiongeza ni mtihani jamani!

 

Kama tungekuwa wapenzi kwa nini tulipelekana hadi polisi kisa kuposti picha yangu kwenye mtandao… hebu wajaribu kuvaa viatu vya wenzao kwa hayo wanayoyatoa mtandaoni,” alisema Kajala ambaye pia ni mama wa mtoto mmoja aitwaye Paula.

 

Kauli ya Kajala imekuja siku chache baada ya kuibuka madai kuwa anatoka na Harmonize ambaye sasa anadaiwa kumwagana na Sarah Michelotti ambaye alidaiwa kuwa mkewe.