HUMPHREY Polepole si jina geni miongoni mwa Watanzania ambao asilimia kubwa vijana ambao wanatamani pia kuwa kama yeye. Ni kijana aliyejijengea jina kutokana na uwezo wake katika kujenga na kutetea hoja.

 

Polepole ambaye sasa ni Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Mbunge mteule wa Bunge la 12 lililozinduliwa Novemba mwaka huu na Rais John Magufuli.

Safari yake katika nyanja ya maendeleo ya vijana ndiyo iliyomuibua kisiasa baada ya Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete kumteua kuwa Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.

 

MTETEZI WA VIJANA

Harakati za utetezi ndani ya jamii hususani vijana ndizo zilizomkuza Polepole licha ya kuwa na ndoto ya  kuwa rubani.

Katika moja ya mahojiano, Polepole alibainisha kuwa ndoto yake ilikuwa kuwa rubani, lakini bahati mbaya uwezo wa familia yake kumudu gharama za masomo hayo ulibadilisha ndoto hiyo.

 

“Nilijikuta kuwa niko active kwenye sekta ya asasi za kiraia licha ya kwamba mwanzoni nilitaka kuwa rubani wa ndege, wazazi walipenda sana iwe hivyo ila kwenye familia mambo yalikwenda chini ndio ikawa nimeshindwa kutekeleza ndoto hiyo,” anasema.

 

Hata hivyo, anasema majukumu ndani ya asasi za kiraia alikuwa anayatekeleza kama ‘hobby’ kwa kuwa hapakuwa na malipo ambayo yangemwezesha kujivunia.

“Nilikuwa active kwenye masuala ya asasi za kiraia na utetezi wa haki za vijana na jamii kwa ujumla. Hili nililifanya kwa sababu ni kitu ambacho kilikuwa kinaniweka bize,” anasema.

 

Licha ya kwamba hobi hiyo ya kujitolea zaidi kwa jamii haikuwa moja ya historia ndani ya familia yao, Polepole ameiendeleza na sasa imekuwa ngekewa kubwa na kioo cha jamii kwa ujumla.

“Kwa sababu baba yangu alikuwa fundi magari, mama maisha yake ni ya nyumbani, hatuna mtu maarufu kwenye familia yetu ambaye ni mwanasiasa, mhamasishaji au mwanaharakati,” anasema.

 

KUJITUMA

Wakati baadhi ya wachambuzi na wadau wakimpongeza katika jitihada zake kwenye majukumu anayopatiwam, Polepole anakiri kuwa alikuwa akijibidisha bila hata malipo.

 

“Nakumbuka miaka ya 2000 mimi na wenzangu tulianzisha asasi moja, ikatuweka bize hadi nikawa nachelewa kurudi nyumba Segerea wakati huo. Sasa bahati mbaya daladala zilikuwa zinaishia Tabata Bima ikishafika saa moja jioni, kwa hiyo nilikuwa nachelewa kurudi nyumba hadi muda mwingine saa sita usiku.

 

“Siku moja baba akaniambia huyo ni bosi gani anakufanyisha kazi namna hiyo hadi usiku… nitakwenda siku moja kumuona. Baba hakujua kama bosi nilikuwa mimi, lakini nashukuru Mungu wazazi wangu walinipatia fursa ya kujifunza mambo mengi,” anasema.

 

SAFARI NDANI YA TUME YA KATIBA

Mwaka 2012, wakati vuguvugu la mabadiliko ya Tume ya Katiba likizidi kupamba mnoto, ndipo aliyekuwa Rais wakati huo, Jakaya Kikwete alitangaza wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba ambayo ilipewa jukumu la kukusanya maoni ya wananchi na kuandaa rasimu ya katiba pendekezwa.

 

Polepole alikuwa mmoja wa vijana waliochomoza ndani ya tume hiyo, iliyokuwa na jumla ya wajumbe 30 pekee, 15 kutoka Bara na 15 kutoka Zanzibar pamoja na viongozi wawili wa Tume hiyo ambayo Mwenyekiti alikuwa Jaji mstaafu Joseph Warioba na makamu Jaji mstaafu Agustino Ramadhani.

 

Hakika huo ndio ulikuwa uwanja wa Polepole baada ya kuzunguka nchi nzima kukusanya maoni na kuyawasilisha kwa Watanzania baada ya kuyachakata.

Kipawa chake cha kuzungumza na kujenga hoja zenye mashiko zilimweka katika ramani nzuri ya kisiasa na kiuongozi nchini.

 

DC MUSOMA, UBUNGO, UENEZI CCM

Kutokana na uhodari wake wa kuchambua mambo, hususani miaka ya 2014 na 2015 ambako kulikuwa na uchaguzi mkuu uliomuingiza madarakani Rais John Magufuli kwa mara ya kwanza, Polepole aliteuliwa kuwa mkuu wa wilaya ya Musoma.

 

Makala zake ndani ya magazeti mbalimbali, pamoja na majukwaa mengine zilizidi kumbeba ambapo aliongoza Musoma kwa miezi miwili pekee kabla ya kuhamishiwa Ubungo ambako nako alihudumu kwa miezi mitano na kuteuliwa kuwa Katibu wa Itikadi na Uenezi CCM.

 

Hakika nafasi hiyo ilizidi kumpa umaarufu mkubwa licha ya kwamba baadhi ya wachambuzi wa kisiasa waliona ni nafasi iliyokuwa ngumu.

Wengi walimfananisha Nape Nnauye ambaye wakati huo aliachia nafasi hiyo baada ya kuteuliwa kuwa Waziri wa Habari, Utamaduni,  Sanaa na Michezo, lakini hawakukumbuka kuwa umbo la Polepole ni tofauti na uwezo wake kiakili.

 

UBUNGE

Novemba 29 mwaka huu, Rais Magufuli  alimteua Polepole kuwa Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ni nafasi ambayo baadhi ya wadau wa siasa wameichukulia kama ASANTE kwa kazi ngumu aliyoifanya kabla ya kampeni, ndani ya kampeni na hata baada ya kampeni za CCM ambazo zimekiwezesha chama hicho kujinyakulia ushindi mkubwa kwa zaidi ya asilimia 80 katika nafasi zote.

 

WACHAMBUZI: ATAFIKA MBALI

Hulka yake iliyojinasibisha na mienendo ya Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere, pia imeigwa na baadhi ya wasomi kama vile Profesa Issa Shivji na Dk. Bashiru Ali.

Mbali na mambo mengine, Dk. Vincent Mashinji ambaye awali alikuwa Katibu Mkuu wa Chadema, anasema alifanya kazi na Polepole akiwa mpinzani na sasa kama kada mwenzie ndani ya CCM.

 

“Hakika Polepole ni kijana mwenye uvumilivu, pili kwa muda mrefu ambao tumefanya naye kazi nimegundua mtu anayependa sana kuona ustawi wa nchi yake ndio maana mawazo yake hayaegemei mahali popote zaidi ya kujali masilahi ya nchi.

 

“Nakumbuka miaka ya 2014, 2015 wakati watu walimtafsiri kama mwanaharakati wa upinzani, kutokana na namna alivyokuwa akikemea na kushauri mambo yaliyokuwa ndani ya serikali, hakuna aliyeamini kama alikuwa mwanachama wa CCM,” anasema.

 

Aidha, anasema wakati anateuliwa katibu wa itikadi na uenezi CCM, hiyo ilikuwa moja ya nafasi iliyokuwa imesheheni majukumu magumu sana kwake.

“Kuwa kwenye nafasi hiyo ndani ya chama tawala ambacho kinapambana katikati ya vita vya kiuchumi palihitaji mtu mtulivu na Polepole alitosha.

 

“Amejitahidi kuwa mtulivu sana na kuhakikisha kujenga taswira nzuri ya Taifa, ni kati ya vijana ambao wanatakiwa kuigwa. Vijana wengine wajifunze usikivu wake, ufanyaji kazi wake. Najua alikuwa na presha kubwa sana ya nje, nakumbuka tulivyofanya kazi kama wapinzani wake, tulikuwa tunamtia presha kubwa sana. Lakini hakuwa na jazba, nadhani ni kijana ambaye kama ataendelea na utulivu huo atafika mbali sana,” anasema.

 

…. ATUMIE UZOEFU KUACHA ALAMA

Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. George Kahangwa anasema ofisi alizopitia Polepole sio jambo baya ni jambo zuri kwa sababu zimemjengea uzoefu mkubwa na uwanja mpana wa mambo.

“Ameona yaliyopo ndani ya harakati, siasa zimempa uwanja mpana na uzoefu mkubwa, tutarajie baada ya fursa zote atakuwa mtu aliyeimarika na kuwa msaada mkubwa kwa taifa,” anasema.

 

Aidha, anasema watanzania sasa wanataka kuona ni kitu gani amelifanyia Taifa.

“Kwa hiyo apate kufanya tafakuri ni nini umefanya kwa Taifa, tunapoandika wasifu wetu huwa tunaandika niliwahi kuwa badala ya kusema niliwahi kufanya hiki na kile kwa mafanikio.

 

“Kwa mfano kuwa Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba pekee haitoshi, je, ameshiriki kutengeneza katiba? Kuwa mbunge haitoshi, je, ameshiriki kutengeneza sheria gani yenye tija kwa taifa? Hayo ndio mambo watanzania wataweza ‘kummic’ katika uzoefu alionao kama kiongozi,” anasema.

 

Anaongeza kuwa Watanzania wanayo ya kusema juu yake, hivyo aendelee kuwasikiliza kwa njia mbalimbali ili kutumia kama kipimo cha utendaji wake.

“Kwa mfano watu wamemjua Polepole kwa kauli mbili tofauti, haina haja kukimbilia kujitetea bali kujitafakari.  Mwisho wa siku ataweza kutengeneza kinachotunza heshima na hadhi yake,” anasema Dk. Kahangwa.

 

POLEPOLE NI NANI

Polepole ni msomi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), kwa mujibu wa maelezo yake anasema alitua Dar es Salaam mwaka 1988 akitokea Tabora. Alisoma shule ya msingi Mbuyuni na kuendelea Shule ya Sekondari Azania, Benjamini Mkapa kisha akajiunga na elimu ya juu huko Arusha na baadaye UDSM.

NA GABRIEL MUSHI