Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba imemshusha kiungo mkabaji raia wa Uganda, Taddeo Lwanga, ambaye amekuja kuchukua nafasi ya Mbrazil Gerson Fraga ambaye alisitishiwa mkataba wake.


Kabla ya utambulisho huo siku chache zilizopita, gazeti dada la Mwanaspoti lilikuwa la kwanza kuripoti ujio wa Lwanga, aliyesaini mkataba wa miaka miwili.


Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Lwanga alisema kuwa amekuja katika kikosi cha Simba kuongeza nguvu pale palipokuwa pamepungua ili kuwa msaada kwa timu kufikia malengo ambayo wamejipangia msimu huu na kwa muda atakaokuwa na timu hiyo.


“Simba ni timu kubwa inayocheza mashindano ya kimataifa, ambayo ina malengo ya kufika mbali, lakini kuna wachezaji wengi wazuri nina imani kwa kushirikiana nao nitatoa mchango wangu ili kuona tunalifikisha guruduma mbali zaidi.


“Kuhusu mambo mengine mengi nadhani nitakuwa na majibu nayo sahihi baada ya kujiunga na timu ambayo hadi wamefikia uamuzi wa kunisajili, kuna kitu ndani yangu wamekiona na ili nisiwaangushe nita waonyesha katika mashindano yote ambayo tutashiriki,” alisema Lwanga.


Lwanga, ambaye mara baada ya kufika katika ofisi za Simba jana, alizungumza na Ofisa Mtendaji Mkuu, Barbara Gonzalez, kisha kuomba apewe jezi namba nne, ambayo awali ilikuwa ikivaliwa na Fraga ila hakufanikiwa kueleza kwa sababu gani ameichagua jezi hiyo.


Katika taarifa hiyo ambayo Simba wameitoa kumalizana na Lwanga, ambaye alikuwa akicheza soka la kulipwa nchini Misri katika klabu ya Tanta, hawakuweka muda wa mkataba wake, lakini tangu awali nyota huyo wa timu ya taifa ya Uganda alishamwaga wino kwa miaka miwili.


Mwenyekiti wa Simba, Mwina Kaduguda, ambaye alikuwa katika picha ya pamoja na Lwanga akiwa anasaini mkataba alisema masuala yote ya usajili katika kikosi hicho kuna watu maalumu, ambao wanasimamia na baada ya kumaliza zoezi hilo taarifa zote zitatolewa na ofisa habari, Haji Manara.