SKENDO ya kuvunjika kwa ndoa ya staa wa Bongo Fleva, Rajabu Abdul ‘Harmonize’ na mkewe, Sarah Michelotti imekwaa kisiki katika kuzima moto wa mwanamuziki Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’, RISASI limedokezwa. Kwa mujibu wa watu wa karibu na wanandoa hao, kuna uwezekano mkubwa, Harmonize au Harmo ametumia skendo hiyo ili kuuzima wimbo mpya wa Diamond au Mondi unaokwenda kwa jina la Waah aliomshirikisha mtu mzima Koffi Olomide au Le Grand Mopao kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Wimbo wa Waah ndiyo habari ya mjini kwani tayari umeweka rekodi za kila aina kwenye anga la muziki wa Afrika. Imeelezwa kwamba, kwa msanii aliyetaka kuusimamisha usiendelee kuwa gumzo, ilibidi itumike nguvu kubwa, jambo ambalo skendo ya Harmo na Sarah imeshindwa kufua dafu.Hadi juzi, Wimbo wa Waah ulikuwa umetazamwa mara milioni 10 ndani ya wiki moja. Wakati wimbo huo ukizidi kukamata, ghafla wiki iliyopita ndipo likaibuka sakata la Harmo kumtambulisha mwanaye, Zulekha aliyezaa nje ya ndoa kwa madai kwamba alikuwa akificha jambo hilo ili kutoharibu uhusiano wake na Sarah, lakini kwa sasa ameamua kuwa mkweli na kumuomba radhi mwanaye huyo kwa kumtelekeza. “Unajua kwa sasa gemu la Bongo Fleva limekuwa gumu mno hivyo wasanii wanatafuta namna yoyote ili wazungumzwe.“Ishu ya Harmonize na Sarah ina shaka kwa sababu ni kwa nini jamaa huyo atangaze sasa wakati ishu ya kuachana kwao ilianza kusikika muda mrefu tu na kuhusu kupata mtoto ilizungumzwa sana kitambo hicho?“ Kuna viashiria vya kwamba ni kiki kwa sababu Sarah bado ameendelea kujitambulisha kama Konde Girl kwenye ukurasa wake wa Mtandao wa Instagram akimaanisha ni binti kutoka Lebo ya Konde Gang Music Worldwide inayomilikiwa na Harmo. “Haiwezekani Sarah agombane na Harmo, halafu aache huo utambulisho wa Konde Girl kwenye ukurasa wake wa Instagram.“Sakata hili limekuja wakati huu kwa sababu mitandaoni kulikuwa kumeshachafuliwa na ngoma ya Mondi ya Waah. “Inawezekana kabisa Harmo ameibua jambo hili akilenga kuhamisha trending (gumzo) mtandaoni.“Lakini mtu aliyesuka mpango huo anakosolewa mno kwani kila kitu kiliharibiwa na Sarah ambaye waraka wake juu ya kuachana na Harmo kupitia ukurasa wake wa Instagram ulijaa walakini mwingi kwamba aliandikiwa. “Pia kuna madai mengine kwamba, baba wa mtoto huyo yupo na alipotaka kujitokeza kuanika ukweli wa ishu hiyo amepoozwa mamilioni ya pesa ili asiharibu mchongo. “Huyu Harmo kuna ushahidi mwingi mno, anapoona kuna mtu anatrendi na yeye anataka kuachia ngoma huwa anafanya mambo ya makusudi ili kuzima ngoma ya mwenzake ili ya kwake itoboe, lakini safari hii amekutana na kina kirefu cha Mondi na kushindwa kufua dafu. “Kuna madai pia kwamba, Harmo alikuwa anataka kuachia Ngoma ya Ushamba Remix akiwa na Naira Marley wa Nigeria.“Itoshe kusema sakata la Harmo na Sarah lina kila dalili ya kutengenezwa,” anasema msanii chipukizi aliyejitambulisha kwa jina la Chinga Boy Rapa mwenye maskani yake Kijitonyama jijini Dar. Akizungumzia sakata hilo, meneja wa Harmo, Beauty Mmari ‘Mjerumani’ alisema kuwa, haamini kama sakata hilo linahusiana na muziki wa msanii wake huyo. “Harmonize ni msanii ambaye anapambana sana ili kuhakikisha anafanya kazi nzuri, sidhani kama jambo hilo lina connection na muziki wake,” alisema Beauty. Harmo na Sarah waliishi kwenye uchumba kwa muda mrefu kabla ya kufunga ndoa ya kimila nyumbani kwa wazazi wa mrembo huyo nchini Italia.Kama hiyo haitoshi, wawili hao waliporejea jijini Dar walifanya bonge la sherehe kisha kuanza kuishi kama mke na mume hadi pale walipopishana na kumwagana. Hivi karibuni, Harmo alidaiwa kuanzisha uhusiano wa kimapenzi na mwigizaji wa Bongo Movies, Kajala Masanja ambaye inaelezwa ndipo anapopoozea machungu mpaka sasa