DAR: Staa wa Bongo Fleva ambaye pia ni mmiliki wa lebo ya muziki Bongo ya Konde Gang Music Worldwide ‘Konde Gang’, Rajabu Abdul Kahali ‘Harmonize’ anadaiwa kufuata ‘uchawi’ nchini Nigeria, IJUMAA limeambiwa.

 

Kwa mujibu wa watu wa karibu wa Harmonize au Harmo, jamaa huyo amekwenda nchini Nigeria kwa ajili ya kujibu pigo la mwanamuziki mwenzake, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’.

 

Imeelezwa kwamba, pigo lenyewe ni Ngoma ya Waah aliyoachia Diamond au Mondi akimshirikisha Le Grand Mopao, Koffi Olomide kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Hivyo, imeelezwa kwamba, Harmo amekwenda kusaka nguvu ya kuzima rekodi za ngoma hiyo ambapo anaamini dawa ni kufanya kolabo ya Wimbo wa Ushamba Remix na msanii wa Nigeria, Naira Marley.

 

 

Kufuatia taarifa hizo kusambaa mitandaoni, baadhi ya mashabiki wa Mondi wamejikuta wakimtolea povu Harmo. “Huyo ndiye Konde Boy; mzee wa kuiga, unaambiwa hataki kufunikwa, anataka awe ndiyo habari ya mjini kila kukicha.

 

“Sasa ameona Simba (Mondi) ameunguruma nyikani na mtu mzima Mopao, naye ameamua kwenda kusaka uchawi wa Kinigeria. Ila siyo mbaya maana anafanya vitu kwa faida na lengo lake ni kutaka kuleta ushindani kwenye gemu,” aliandika mmoja wa wafuasi wa Harmo kwenye Mtandao wa Instagram.

 

 

Ili kupata undani wa ishu hiyo, Gazeti la IJUMAA lilizungumza na Meneja wa Harmo, Beauty Mmary ‘Mjerumani’ ambapo alifunguka kuwa, mashabiki wake watarajie jambo kubwa kutoka kwa Harmo na msanii huyo wa Nigeria. “Ni kweli hiyo projekti ipo ya kufanya kazi na Naira Marley hivyo mashabiki wakae mkao wa kula,” alisema meneja huyo.

 

Inafahamika kwamba, tangu mwaka jana Harmo alipojitoa Lebo ya Wasafi Classic Baby (WCB) iliyo chini ya Mondi hajawahi kuwa na maelewano mazuri na bosi wake huyo wa zamani na hata wanapokutana hawakai karibu. Harmo na Mondi ni wasanii ambao wamekuwa kwenye ushindani mkubwa kwenye kupitia muziki wao, lakini Harmo amekuwa akikosolewa mno kwamba, yeye siyo levo moja na Mondi hivyo asijilinganishe naye.

Stori: Khadija Bakari