INASHTUA! Jaji mmoja nchini Kenya amekutwa na umauti hivi karibuni akiwa nyumbani kwa mchepuko alikokwenda kupoza moyo.

 

Taarifa za polisi nchini humo zinamtaja jaji huyo kuwa ni Godfrey Hillary Oduor ambaye alikuwa akihudumu katika Mahakama ya Kisumu. Inaelezwa kuwa, jaji huyo alifia nyumbani kwa mchepuko aliyejajwa kwa jina la Njoki Muhia.

 

Kwa mujibu wa ripoti ya polisi, kifo cha Oduor kiliripotiwa na Njoki, Alhamisi Disemba 17, mwaka huu, baada ya kurejea nyumbani na kumkuta mpenzi wake akiwa amekata roho.

 

Taarifa ya polisi inaeleza kuwa Njoki alirejea nyumbani katika mtaa wa Riverbank Estate-Phase 2 South B kutoka kazini na kukuta mlango wa chumba chake ukiwa umefungwa kwa ndani.

 

Baada ya kuhangaika kwa muda mrefu kutafuta namna ya kuingia ndani, Njoki aliamua kuchungulia dirishani ambapo alimuona mpenzi wake akiwa amelala kitandani huku povu likimtoka mdomoni.

 

Hisia za kuwepo kwa tukio lisilokuwa la kawaida lilimwingia na kuamua kupiga simu katika Kituo cha Polisi cha Hazina ambapo maofisa wake walifika na kumkuta Oduor akiwa amekata roho.

 

Akisimulia mkasa huyo Njoki alisema hajui ni kitu gani kilimpata mpenzi wake ambapo alikiri kuwa amekuwa akiishi naye kwa muda mrefu.

 

Hata hivyo, haikufahamika mara moja jaji huyo anaishi wapi na familia yake na kwamba nini kilimsibu hadi kuamua kuhamia kwa hawara ambaye alikuwa akiishi kwenye chumba kimoja cha kupanga.

 

Jaji Mkuu wa Kenya David Maraga alituma rambirambi zake kwa jamaa na marafiki wa Oduor akisema jaji huyo alikuwa akifanya kazi yake kwa weledi.

 

Kifo cha jaji Oduor kimekuwa gumzo nchini humo huku kila mmoja akieleza yake, lakini polisi wamejizuia kusema chochote mpaka watakapokamilisha uchunguzi wao.

STORI: MWANDISHI WETU NA MITANDAO