KWA hali jinsi ilivyo inaonekana wazi aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Klabu ya Simba, Hassan Dalali ametolewa nje ya boksi katika uchaguzi mdogo wa klabu hiyo unaotarajiwa kufanyika Februari 7, mwakani kutokana na kutokidhi vigezo.

 

Simba inatarajia kufanya uchaguzi mdogo Februari 7, mwakani kuziba pengo la aliyekuwa mwenyekiti wa klabu hiyo, Swed Mkwabi ambaye alijiuzulu Septemba mwaka jana kutokana na sababu zake binafsi huku nafasi hiyo ikikaimiwa na mjumbe wa bodi ya wakurugenzi ndani ya Simba, Mwina Kaduguda.

 

Wagombea 11 ndiyo waliojitokeza kuchukua fomu za kuwania nafasi hiyo muhimu ndani ya Simba huku saba kati ya hao ndiyo waliorudisha fomu na wanne wameshindwa kurudisha.

 

Awali, wagombea waliojitokeza ni pamoja na Hassan Dalali, Juma Nkamia, Victor Anton, Rashid Shangazi, Ayubu Semvua, Mohamed Soloka, Kassim Manyagalika, Afred Elia, Hamis Omary, Mutaza Mangungu na Piton Mwakisu.

 

Akizungumza na Championi Jumamosi,Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi Simba, Boniface Lihamwike alisema kuwa, moja ya sheria itakayotumika katika usaili huo ni wagombea kuonyesha cheti cha shahada ‘digrii’ na iwapo mgombea hatakuwanacho anaondolewa katika mchakato huo, Hivyo kutokana na kigezo hicho moja kwa moja kinamuondoa Dalali katika kinyang’anyiro hicho kutokana na kuwa na elimu ya kidato cha nne.

 

“Tayari wajumbe wamesharudisha fomu za kuwania nafasi ya uenyekiti ndani ya Simba ambapo miongoni mwa wajumbe 11 waliojitokeza, saba pekee ndiyo wamerudisha fomu akiwemo Nkamia, Dalali, Mutaza, Shangazi, Mwakisu na majina mengine kidogo yamenitoka na wasiorudisha ni Semvua, Victor na Nyangalika.“

 

Tunawafanyia usaili wagombea tarehe 27 (kesho) na 28 kwa kuzingatia vigezo tulivyoviweka ambavyo ni cheti cha digrii na umri.

 

Mgombea akiwa na umri kuanzia miaka 65 hatokuwa na kigezo cha kuwania nafasi hiyo, pia kanuni haimruhusu mtu mwenye elimu ya kidato cha nne, sita na diploma (stashahada), hivyo kama mtu hatakuwa na cheti cha digrii ataondolewa katika kinyang’anyiro hicho,” alisema Lihamwike

Stori na Khadija Mngwai, Dar es Salaam