Mwanasaikolojia Moses Kyando amesema kuwa kitendo cha mteule wa Rais Magufuli, Francis Ndulane, kushindwa kuapa lisihusishwe na masuala ya kishirikina bali ni masuala ya kisaikolojia aina ya Specific Phobia na Social Phobia, yanayoweza kumpata mtu yeyote.


Kauli hiyo ameitoa hii leo Decemba 10, 2020, wakati akizungumza kwenye kipindi cha SupaBreakfast ya East Africa Radio, ambapo amesema kiongozi huyo siyo wa kushindwa kuapa kwa kuwa hata CV yake inaonesha kuwa ni msomi na alishawahi kuwa kiongozi wa bodi mbalimbali.


"Kilichompata Naibu Waziri mteule wengi wanasema ni uchawi ama hajui kusoma na kuandika lakini ukiangalia CV yake siyo mtu wa kushindwa kusoma, amefanya kazi nyingi za kijamii, kitaalam hayo ni masuala ya kisaikolojia ambayo ni Social Phobia na Specific Phobia, sasa unapokutana na Rais ambaye ana mambo mengi na baadhi ya watendaji wanapata naye shida inawezekana alikutana na phobia mbili kwa wakati mmoja", amesema Mwanasaikolojia


"Inawezekana hata watu wake wa karibu wakimuuliza na yeye anashangaa ni tatizo la kisaikolojia ambalo linaweza kumpata mtu wa aina yoyote, ni hofu kupanda juu ya jambo ambalo hukulitegemea, kwa jana kulikuwa na mkusanyiko wa watu wamevaa suti na Rais Magufuli alikuwepo, unaweza kukuta kilichompata jana ni phobia, yeye ni mtu wa kawaida na ni msomi na hana changamoto ", ameongeza.


Jana Decemba 9, 2020, Naibu Waziri mteule wa Madini Francis Ndulane, alishindwa kula kiapo mbele ya Rais Magufuli , na baada ya hapo Rais Magufuli, alitangaza kuwa nafasi hiyo atateuliwa mtu mwingine na itabidi mteule huyo elimu yake ichunguzwe.