Chadema imeanza kutumia nguvu ya mahakama kupinga mchakato wa uteuzi wa wabunge 19 wa viti maalumu na mtu aliyesaini fomu zao kwa nafasi ya katibu mkuu.


Chama hicho kilistahili kupata wabunge wa viti maalum kutokana na kupata idadi ya kura za wabunge inayozidi asilimia tano, lakini kinadai hakukuwa na kikao kilichopitisha majina ya wanachama na kupeleka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kwa ajili ya uteuzi.


Lakini Noveemba 24, makada 19 walijitokeza viwanja vya Bunge na kuapishwa kuwa wabunge wa viti maalumu katika utaratibu mpya unaomruhusu Spika kufanya kazi hiyo bila ya kuwepo na mkutano wa chombo hicho cha kutunga sheria, kitendo kilichosababisha Kamati Kuu ya Chadema iliyokutana Novemba 27 kuamua kuwavua uanachama.


Pamoja na kustahili viti hivyo, Chadema ilishatangaza kutotambua matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 28, ikidai kwamba uchaguzi huo ulitawaliwa na ukiukwaji wa sheria na taratibu.


Mkurugenzi wa itikadi, uenezi, mawasiliano na mambo ya nje wa Chadema, John Mrema alisema mchakato huo unaendelea na tayari katibu mkuu wa chama hicho, John Mnyika ameiandikia barua NEC.


Katika barua hiyo kwa NEC, alisema Chadema inataka kupatiwa nakala ya barua iliyowasilisha majina pamoja na fomu namba 8D ambazo katibu mkuu anatakiwa kujaza ili ijulikane aliyeijaza na hivyo aunganishwe kwenye kesi hiyo.


“Hatujapata majibu. Mawakili wanaendelea na utaratibu wa kufungua shauri,” alisema Mrema alipozungumza na gazeti hili jana.


Pia Mrema alisema chama chake kimemwandikia barua Spika wa Bunge, Job Ndugai kumjulisha uamuzi wa Kamati Kuu wa kuwavua uanachama wabunge hao 19 wa viti maalumu.


Alisema wameamua kufanya hivyo ili kuweka wazi kwamba nafasi 19 za viti maalumu za Chadema bado ziko wazi ili Spika asije akawatambulisha makada hao wa zamani kama ni wabunge wa Chadema.


“Baada ya kuwafukuza, Jumatatu (Novemba 30) tukapeleka barua kwa Spika kumtaarifu uamuzi wa Kamati Kuu tukitegemea mpaka sasa Spika atakuwa ameipokea hiyo barua na kuijulisha Tume ya Uchaguzi,’’ alisema.


Hata hivyo, alipoulizwa na Mwananchi jana kama amepokea barua hiyo, Spika Ndugai alisema: “Nipo jimboni. Kama kweli wameandika barua mwambie huyo Mnyika aniletee mkono kwa mkono. Hilo ndio jibu langu.”


Kuhusu Chadema kupeleka barua hiyo kwa Spika ambaye amepatikana katika uchaguzi ambao wanadai hawautambui, Mrema alisema wamelazimika kufuata sheria kwa sababu yeye ndiye Spika aliyepo.


“Hata kama hatumtambui, ndiyo Spika aliyepo. Kwa hiyo hakuna Spika mwingine ambaye tungeweza kumpelekea. Kwa hiyo, kwa mujibu wa sheria na taratibu tumempelekea.


“Lazima tumtaarifu ili aijulishe Tume. Akiamua kutoitaarifu Tume ya Uchaguzi sasa hilo si tatizo letu, ni suala la kujua kwamba Chadema haina wabunge wa viti maalumu.”


Mrema alisema uamuzi wa kuwafukuza uanachama wabunge hao haujabatilishwa, kwa kuwa ni halali mpaka pale rufaa yao itakaposikilizwa na kuamuliwa vinginevyo na Baraza Kuu. Alisema bado wanasubiri rufaa zao na wana siku 30 za kufanya hivyo tangu walipofukuzwa.


“Tunaendelea kusubiri rufaa zao. Bado wana muda, wana siku 30 za kukata rufaa. Kwa hiyo tunasubiri kama watakuja,” alisema Mrema.


Alipoulizwa lini kikao cha Baraza Kuu kitakaa kusikiliza rufaa, Mrema alisema kuna utaratibu wa kuitisha kikao baada ya kupokea rufaa, lakini kwa utaratibu wa kawaida Baraza Kuu lilitakiwa kukutana Machi 2021.


“Kwa sasa siwezi nikakwambia kikao cha Baraza Kuu kitafanyika lini kwa sababu hata hizo rufaa zenyewe bado hatujazipata. Lakini kikao ca Baraza Kuu cha kawaida kitakuwa Machi mwakani. Tukipokea rufaa basi kikao kitaitishwa,” alisema.


Gazeti hili lilimtafuta Halima Mdee, aliyekuwa mwenyekiti wa Baraza la Wanawake (Bawacha) na ambaye ni mmoja wa wabunge hao 19 waliovuliwa uanachama, ili azungumzie rufaa yao au kwenda mahakamani kupinga uamuzi wa Kamati Kuu, lakini jitihada ziligonga mwamba na hata alipopigiwa simu, hakupokea simu wala kujibu ujumbe mfupi.