Jeshi la Polisi mkoani Tabora, limefanikiwa kuwakamata jumla ya watuhumiwa 683 kwa makosa mbalimbali katika Oporesheni ilichukua wiki tatu katika Wilaya zote za Mkoa huo.

Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Opereshemi Maalumu za Jeshi la Polisi Tanzania, Kamishina Mwandamizi wa Jeshi wa Polisi (SACP) Mihayo Msikhela, wakati akizungumza na waandishi wa Habari Tabora.

Amesema miongoni mwa watuhumiwa hao, 277 wamefikishwa Mahakamani na kuhukumiwa, watuhumiwa 255 bado kesi zao zinaendelea na watuhimiwa 42 wako katika uangalizi wa Polisi baada ya kutokuwepo kwa ushahidi madhubuti.

SACP Msikhela amebainisha kuwa, baadhi ya vielelezo vilivyokamatwa ni silaha aina ya gobore moja, mapanga tisa, meno ya tembo mawili, pikipiki 34 , magodoro 10 na simu za mkononi nne, vyuma vya reli viwili, runinga za aina mbalimbali 19, mfano wa sare za majeshi mbalimbali ya ndani na nje na pombe haramu ya gongo lita 408.