Rais wa zamani wa Burundi Pierre Buyoya amefariki akiwa na umri wa miaka 71 ,binamu yake na chanzo cha kidiplomasia chathibitishia BBC.

Chanzo cha familia kimesema alifariki mjini Paris, Ufaransa siku ya Alhamisi kutokana na athari za ugonjwa wa Covid-19.

Jenerali huyo mstaafu alihudumu mara mbili madarakani kwa jumla ya miaka 13 baada ya kumpindua watangulizi wake madarakani

Mwezi Oktoba, alihukumiwa kifungo cha maisha gerezani na mahakama ya Burundi kwa kosa la mauaji ya rais wa kwanza aliyechaguliwa kidemokrasia nchini, Rais Melchior Ndadaye mwaka 1993 - ambayo yalisababisha mauaji ya karibu watu 300,000. Alikana kufanya makosa

Mwezi uliyopita, alijiuzulu kama mjumbe wa Muungano wa Afrika wa eneo la Sahel, na kusema kuwa anataka kutumia muda wake zaidi kusafisha jina lake.