Samirah Yusuph
WAJUMBE wa Bodi mpya ya Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira mjini Maswa (Mauwasa)katika wilaya ya Maswa mkoani Simiyu wametembelea bwawa la New Sola lililoko katika kijiji cha Zanzui.

Bwawa hilo ndicho chanzo kikuu cha maji kwa wakazi wa mji wa Maswa na vijiji 11 na linahudumia zaidi ya wakazi 100,000 pamoja na mifugo zaidi ya 400,000 na liko chini ya Mamlaka hiyo.

Wajumbe hao ambao wakiongozwa na Mwenyekiti wa bodi hiyo,Pauline Ntagaye  pia waliweza kutembelea mitambo ya kusukuma maji iliyoko kwenye bwawa hilo na kujionea jinsi maji yanavyotibiwa na kuondolewa tope kabla ya kusukumwa kwenda kwa watumiaji wa maji hayo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Mauwasa,Mhandisi Mathias Nandi aliwaeleza wajumbe hao kuwa  wamekuwa wakikabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo gharama za uendeshaji kuwa kubwa kuliko makusanyo kwa mwezi .

Alisema kuwa tangu Mamlaka hiyo uanze kufanya kazi mwaka 1990 bado wanatumia mitambo hiyo ambayo kwa sasa imechakaa na hivyo imekuwa ikifanyiwa ukarabati wa mara kwa mara hivyo kusababisha kusitisha utoaji wa huduma ya maji kwa wateja wao.

"Gharama tunazotumia katika uendeshaji wa Mamlaka ni kubwa kulingana na mapato yetu tunayokusanya kwa mwezi kwani tunatumia gharama kubwa ya kununua madawa ya kutibu maji na kuyasafisha ili kuondoa tope pamoja na gharama za umeme,"

"Hata hizi mashine tunazotumia kuvutia maji katika bwawa tunazo mbili tu na kwa sasa  mashine moja imeungua,tunatumia moja nayo ikiungua tunasitisha huduma na hizi ni za muda mrefu tangu mamlaka ilipoanzishwa mwaka 1990 zimechakaa ila tunajitahidi kuzifanyia ukarabati mara kwa mara lakini gharama ni kubwa,"alisema.

Pia alisema kuwa baadhi ya wananchi wamekuwa wakivamia eneo la hifadhi ya bwawa hilo kwa kuingiza mifugo na wanapothibitiwa na walinzi lakini wamekuwa wakiwashambulia kwa kutumia silaha za jadi hadi hapo wanapohitaji  msaada kwa jeshi la polisi.

Aliongeza kueleza kuwa wananchi wote waliokuwa na maeneo katika eneo la hifadhi ya bwawa hilo kwa sasa wote wameshalipwa fidia kwa hiyo hakuna mwananchi hata mmoja ambaye anaidai Mamlaka hiyo juu ya fidia ya maeneo.

Mwenyekiti wa bodi ya Mauwasa,Paulina Ntagaye alisema kuwa sasa ufike mahali serikali ikaiangalia Mamlaka hiyo kwa jicho la huduma kwa kuisaidia kupata mitambo mipya ya kusukuma maji ili waweze kuwahudumia wateja wao kwa kuwapatia huduma bora ya maji safi na salama.

"Ni kweli Mamlaka yetu mitambo yetu imechakaa hasa ya kusukuma maji ni vizuri serikali ikatusaidia kupata mitambo mipya ili tuweze kutoa huduma bora kwa wananchi wa mji wa Maswa ukizingatia kuwa hiki ndicho chanzo kikuu cha maji,"alisema.

Aidha aliwaomba wananchi wa vijiji wanaolizunguka bwawa hilo kuheshimu sheria zilizowekwa za kuzuia kufanya shughuli za kibinadamu katika hifadhi ya bwawa hilo kwani watakaokamatwa sheria itachukua mkondo wake na wako tayari kulilinda bwawa hilo kwa gharama yoyote.

MWISHO.