Mgombea wa kiti cha urais kupitia chama cha NUP Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine amekamatwa na jeshi la UPDF kwenye kisiwa cha Kalangala akiwa katika kampeni zake za uchaguzi.
Kulingana na msemaji wa chama cha NUP Joel Ssenyonyi amekamatwa na timu yake aliyokuwa akiongozana nayo wakiwemo wandishi habari.

Mwandishi wa BBC Issaac Mumena amezungumza na msemaji wa chama cha NUP Joel Ssenyonyi na kuthibitisha kukamatwa kwa mgombea huyo.

Bobi Wine ameanza kampeni zake leo baada ya kupumuzika kwa muda wa siku tatu tangu kutokea kwa kifo cha mlinzi wake na kujeruhiwa kwa waandishi habari watatu mwishoni mwa juma.

Kyagulanyi alipanda boti kwenda kisiwa cha Kalanga kuanza kampeni zake leo asubuhi.

''Siku ya leo mgombea wetu wa kiti cha urais mheshimiwa Robert Kyagulanyi Ssentamu alikuwa amekwenda katika kampeni zake kisiwani Kalangala, ndiyo ratiba yake inavyoonyesha akiwa amefuatana na tume ya uchaguzi. Jeshi la polisi limemkamata na timu yake ya watu karibu 90. Hatujui wamewapeleka wapi na kwanini wamewakamata na hakuna anayezungumuza nao, hiyo ndio hali halisi ilivyo na inatia wasiwasi na kuogopesha'', ameeleza Joel Ssenyonyi.

Hata hivyo, naibu msemaji wa jeshi la polisi Luteni Kanali Deo Akiiki amekataa kusema chochote kuhusu tuhuma hizo.

''Operesheni zote tunazofanya ni operesheni ya pamoja ya uchaguzi mkuu inayongozwa na jeshi la polisi. Kila unachokiona sijui Kyagulanyi au wafasi wa Kyagulanyi, polisi ndiyo wanaotakiwa kulizungumzia siyo jeshi'', Bwana Deo Akiiki amesema.

Katika mtandao wa kijamii jeshi la polisi limekanusha kumkamata Bobi Wine lakini likasema kuwa kilichofanyika ni kwamba wamemuzuia kufatana na mkusanyiko mkubwa watu ili kutekeleza kanuni za watalaam wa afya za kuzuia kusambaa kwa virusi vya corona.

Inasemekana Bobi Wine anatarajiwa kurudishwa nyumbani kwake sehemu ya Magele kwa helikopta ya jeshi kutoka kisiwani Kalangala.