Rais wa Tanzania,  John Magufuli  jana Jumamosi Desemba 5, 2020 amefanya uteuzi wa mawaziri 21 na naibu mawaziri 23 huku akiwateua waliokuwa makatibu wakuu wa wizara kuwa wabunge na kisha kuwateua kuwa mawaziri.Pia  ameanzisha wizara mpya ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari na kumteua mbunge wa Kigamboni, Dk Faustine Ndugulile kuwa waziri wa wizara hiyo na Kundo Mathew kuwa naibu waziri.


Akitangaza uteuzi huo katibu mkuu kiongozi, Balozi John Kijazi amesema uteuzi wa mawaziri wawili, Profesa Palamagamba Kabudi (Mambo ya Nje) na Dk Philip Mpango (Fedha) unaendelea na hivyo kufanya idadi ya mawaziri kuwa 23 na naibu mawaziri 23.

Walioteuliwa kuwa wabunge na kisha uwaziri ni Dk Dorothy  Gwajima aliyekuwa naibu katibu mkuu Tamisemi akishughulikia sekta ya afya pamoja na Dk Leonard Chamuriho ambaye alikuwa katibu mkuu Wizara ya Uchukuzi.