Waziri wa madini Doto Biteko, amebainisha kuwa changamoto na mvutano uliopo baina ya Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), unapaswa kufika ukomo ili shughuli za uchimbaji makaa ya mawe uweze kusonga mbele.

Waziri wa Madini Doto Biteko, ameeleza mpango huo wa serikali wakati akizungumza kwenye kikao kazi na watumishi wote wa Wizara hiyo kilichofanyika katika Mji wa serikali Mtumba Jijini Dodoma, na kuongeza kuwa serikali imeeleza dhamira yake ya kuanza uchimbaji wa makaa ya mawe kupitia Shirika la Madini la Taifa (STAMICO).


"Tutakuwa na urafiki mahali tutakapokuwa tunafanya vizuri na kununiana pale ambapo hatutafanya vizuri na mimi kiu yangu ni kuona wote tunafanikiwa", amesema Biteko


Awali Waziri Biteko amewaasa watendaji wa Wizara hiyo ya Madini kubadilika kutokana na mazingira, kwani mazoea waliyokuwa nayo kabla ya uteuzi wa Naibu Waziri yanapaswa kumalizika na kulinda heshima ya viongozi hao.


"Mazoea siyo mahala pake kwa sasa, na mkiona Mh. Rais, amemteua kiongozi kutoka kwenye Wizara ya Madini maana yake ameona utendaji uliotukaka kwani ana Watanzania wengi wenye uwezo wa kufanya kazi kwa weledi lakini wakati mwingine anatoa upendeleo", amesema Waziri Biteko.