Umoja wa Afrika unasema hatua ya Somalia, kuvunja uhusiano wa kidiplomasia na Kenya, unahatarisha usalama na uthabiti wa eneo la Afrika Mashariki na pembe ya Afrika.

Kauli hii imetolewa na rais wa Tume ya Umoja huo Moussa Faki Mahamat, baada ya viongozi kutoka mataifa ya IGAD, kukutana nchini Djibouti mwishoni mwa wiki iliyopita, kujaidliana kuhusu mvutano huo.

Haya yanajiri wakati rais wa Kenya Uhuru Kenyatta alikutana ana kwa ana na mwenzake wa Somlia Mohamed Abdullahi ambaye wiki iliyopita, alivunja uhusiano na Kenya kwa madai kuwa nchi hiyo inaingilia siasa zake za ndani kuelekea uchagauzi Mkuu mwaka ujao, madai ambayo Kenya imekanusha.

Siku ya Jumatatu rais wa Kenya Uhuru Kenyatta alikutana na kufanya mazungumzo na rais wa jimbo linalojitegemea na ambalo lilitangaza kujitawala la Somaliland Muse Bihi Abdi.

Uongozi wa Mogadishu pia umekuwa ukiishtumu Kenya kwa kumuunga mkono rais wa jimbo la Jubaland, Ahmed Madobe, ambaye ana uhusiano mzuri na rais wa nchi hiyo Mohamed Abdullahi Farmajo.

Mzozo huu unajiri wakati huu nchi hizo zikiendelea kutegemeana katika masuala ya kiuchumi pamoja na usalama kutokana na jeshi la Kenya, KDF, kuwa nchini Somalia kusaidia katika vita dhidi ya kundi la kigaidi la Al Shabab.

 

Credit: RFI