Rais wa chama cha ngumi za kulipwa cha WBF Howard Goldberg atawasili nchini Jumatano kwa ajili ya usimamizi wa pambano ubingwa wa mabara super-welterweight  kati ya bondia Hassan Mwakinyo na Jose Carlos Paz wa Argentina lililopangwa kufanyika kwenye ukumbi wa Next Door Arena, Oysterbay Ijumaa Novemba 13.

Goldberg atawasili pamoja na mwamuzi wapambano hilo Edward John Marshall saa 3.15 asubuhi kwa ndege ya shirikala ndege la Kenya, KQ.

Mbali ya kuwa Rais wa WBF, Goldberg enzi zake alikuwa mwamuzi na jaji wa ngumi za kulipwa duniani akiwa amecheza zaidi yapambano 300 katika nchi mbalimbali.

Goldberg anakuja nchini kwa mara ya sita kwa ajili ya kusimamia ngumi za kulipwa na amefurahishwa sana na weledi wa kampuni ya Jackson Group Sports  katika pambano hili kwani wamekwisha kamilisha masharti yote ikiwa pamoja na tiketi za ndege za ujio wao.

Alisema kuwa kampuni ya Jackson Group Sports imeonyesha njia chanya katika kuandaa mapambano ya ngumi za kulipwa kwa weledi na uwazi mkubwa, jambo ambalo limewafanya wao kutoa kibali na kuja kusimamia pambano la Mwakinyo dhidi ya Paz.

Alisema kuwa kila kitu ambacho WBF ilikiitaji kutoka kwa waandaaji wa pambano hilo kilipatikana na kukamilishwa haraka, jambo ambalo limewapa faraja kubwa.

Kwa mujibu wa Goldberg, ujio wa Jackson Group Sports kwenye ngumi ni fursa kwa mabondia wenye lengo la kupata maendeleo na anaamini Tanzania (kupitia Jackson Group Sports) itapata mabondia wengi wenye vipaji.

Alisema kuwa ametembelea nchi zaidi ya 60 duniani kwa kazi kusimamia mapambano ya WBF, lakini amekuwa na furaha zaidi kuja Tanzania yenye vivutio vikubwa vya utalii ikiwa pamoja na hifadhi ya Serengeti na Zanzibar.

“Nimekuwa niliulizwana baadhi ya maofisa wa WBF kwa nini napendakuja Tanzania, jibu ni rahisi sana, ni nchi yenye uzuri wa asili na vivutio vingi vya utalii, wananchi wake wana upendo mkubwa na ushirikiano ambao nimekuwa nikiupata na serikali kupitia Wizara ya Michezo na mapromota,” alisema Golberg.

Wakati huo huo; mabondia Fatuma Zarika atawasili nchini leo kwa ajili ya pambano lake dhidi ya Patience Mastara wa Zimbabwe ambaye atawasili (Jumanne) usiku.

Mkurugenzi wa Jackson Group Sports, Kelvin Twissa alisema kuwa Zarika atawasili saa 3.30 usiku tayari kwa pambano hilo. Tayari Mpinzani wa bondia Hassan Mwakinyo, Paz amewasili nchini na anaendelea kujifua.

Alisema kuwa mabondia wengine, Alex Kabangu kutoka Dr Congo ambaye atazichapa na Hussein Itaba wa Tanzania atawasili kesho (Jumanne) usiku huku mpinzani wa bondia Zulfa Macho wa Tanzania, Alice Mbewe atawasili nchini leo.

Twissa alisema kila kitu kiko katika hatua za mwisho na tiketi zitaanza kuuzwa kwa njia ya Nilipe na Selcom kwa Sh 3 Milioni kwa meza ya watu 10 na  Sh150,000 kwa kwa viti vya kawaida.
Hassan Mwakinyo akiwa na bondia  Zulfa Macho. mabondia hao wapo katika maandalizi kwa ajili ya kuzichapa na wapinzani wao Novemba 13 kwenye ukumbi wa Next Door Arena, Oysterbay.

Bondia Jose Carlos Paz (kulia) akiwasili pamoja na kocha wake, Alberto Ramon.