WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amezindua kazi ya uchepushaji maji ya mto Rufiji kwenda kwenye handaki ili kupisha ujenzi wa tuta kuu la bwawa la kufua umeme na kusema mradi huo utawezesha nchi kuwa na umeme mwingi na wa kutosha lakini pia utawezesha kufanya biashara ya umeme na nchi za jirani.

Ametoa kauli hiyo leo mchana (Jumatano, Novemba 18, 2020) wakati akizungumza na wananchi na wadau mbalimbali waliohudhuria uzinduzi huo kwenye eneo la mradi, mkoani Pwani wakati akikagua maendeleo ya utekelezaji wa mradi wa uzalishaji umeme kwa kutumia maporomoko ya mto Rufiji.

“Upatikanaji wa umeme wa bei nafuu na uhakika nchini kwetu utachochea ukuaji na mapinduzi katika sekta ya viwanda nchini kwa kushusha gharama za uendeshaji viwandani, kukabiliana na mfumuko wa bei, kuwezesha ushindani wa bidhaa za Tanzania katika masoko ya Afrika Mashariki, Afrika na duniani,” amesema.

Amesema hatua hiyo itaenda sambamba na kuvutia uwekezaji mkubwa, wa kati na mdogo katika sekta mbalimbali nchini kutokana kupungua kwa gharama za umeme katika uzalishaji ikiwa ni pamoja na kuwawezesha Watanzania wote kumudu gharama za umeme mijini hadi vijijini.

Waziri Mkuu amesema mradi huo ambao unafadhiliwa na Serikali kwa asilimia 100 kwa gharama ya sh. trilioni 6.557, unasimamiwa na Mhandisi Mshauri wa Kitanzania kwa asilimia 100. “Serikali imeendelea kuwaamini na kuwatumia wataalamu wa Kitanzania katika kusimamia miradi mikubwa, na kwa kutambua hilo mradi huu unasimamiwa na Mhandisi Mshauri wa Kitanzania kwa asilimia 100,” amesema.

Amesema mradi huo wa kufua umeme kwa kutumia maji wa Julius Nyerere ni mkubwa, wa kimkakati na wa aina yake katika ukanda wa Afrika, ukiwa ni wa kwanza kwa ukubwa kwa Afrika Mashariki na wa nne barani Afrika na akasisitiza kuwe na usimamizi makini na wa viwango ili kuhakikisha unakamilika katika muda uliopangwa.

“Nimeambiwa kwamba, mradi huu unaenda sambamba na ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme ya msongo wa kilovoti 400 kutoka eneo la mradi hadi Chalinze, yote hii ni kuhakikisha umeme unaotoka hapa unaingizwa kwenye gridi ya Taifa.”

Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na washiriki wa hafla hiyo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Zena Said alisema hadi kufikia Oktoba 31, mwaka huu, mradi huo ulikuwa umeshatoa ajira za moja kwa moja 6,364 ambapo kati ya hizo, ajira 5,728 zikiwa ni za Watanzania.

Akielezea hatua iliyofikiwa kwenye usambazaji wa umeme nchini, Katibu Mkuu huyo alisema kwamba hadi sasa vijiji 9,884 kati ya 12,264 viliyopo nchini vimekwishapatiwa umeme. “Tuna mpango wa kukamilisha vijiji vyote vilivyobakia ndani ya miaka miwili ijayo,” alisema.

Wakati huohuo, Waziri wa Nyumba na Huduma za Mijini wa Misri, Dkt. Assem el Gazzar amesema Rais wa nchi hiyo, Abdel Fattah al-Sisi anafuatilia kwa karibu utekelezaji wa mradi huo ambao unajengwa kwa ubia na kampuni za Arab Contractors and El Sewedy Electric kutoka Misri.

“Rais wetu anafuatilia kwa karibu maendeleo ya mradi huu na tunatarajia utaisha ndani ya muda uliopangwa. Kukamilika kwa mardi huu kutahakikisha nishati ya umeme inakuwa ya uhakika katika kuleta maendeleo,” alisema.

Katika hatua nyingine, Waziri wa Umeme na Nishati Jadidifu wa Misri, Dkt. Mohamed Shaker El-Markabi alisema Serikali ya nchi hiyo iko tayari kubadilishana uzoefu na wizara ya nishati ya Tanzania na kwamba itatoa mafunzo kwa Watanzania 25 kwa miaka mitatu ijayo.

“Tunawapongeza Watanzania kwa hatua hii ya kihistoria. Wizara yetu iko tayari kubadilishana uzoefu na kujengeana uwezo na Wizara ya Nishati ya Tanzania, na katika kipindi cha miaka mitatu ijayo, tutatoa mafunzo (full training) kwa Watanzania 25,” alisema.

Alisema upatikanaji wa umeme wa uhakika ni suala la muhimu kwa wananchi kama ilivyo kwa maji na huduma nyingine muhimu. “Uzalishaji wa megawati 2,115 utaiwezesha Tanzania kuwa na umeme wa uhakika, itaongeza kiwango cha upatikanaji wa umeme na kutengeneza fursa za ajira na za kibiashara.”

“Ndani ya miaka mitatu ijayo, Tanzania itakuwa kinara wa uzalishaji nishati katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati. Mradi wa umeme wa Julius Nyerere (JNHPP) utakapokamilika, unatarajiwa uweze kutoa ziada ya kuuza kwenye nchi za jirani,” alisema.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa TANESCO, Dkt. Tito Mwinuka alisema ujenzi wa mradi huo umefikia asilimia 75.76 na kwamba uchepushaji wa maji ya mto uliofanyika sasa ni wa muda tu ili kupisha ujenzi wa tuta kuu. “Tumekwepesha umbali wa mita 700 tu, na tukimaliza ujenzi wa tuta, tutarudisha maji ya mto kwenye njia yake ya awali,” alisema.