Mwenyekiti TLB Manispaa ya Iringa David Mgimwa akizungumza na waandishi wa habari juu la ombi lao la kupewa elimu ya magonjwa ya milipuko.


Na Fredy Mgunda,Iringa.

CHAMA cha watu wenye ulemavu wa macho TLB Mkoani Iringa kimeeleza kuwapo kwa hofu juu ya wanachama wake kuambukizwa magonjwa ya milipuko kutokana na kundi hilo kutopatiwa elimu ya kujikinga magonjwa hayo.

Mwenyekiti wa TLB mkoani Iringa Huruma Maketa alisema tangu kuibuka kwa maambukizi ya virusi vya Corona vinavyosababisha ugonjwa wa Covid 19 nchini kundi la walemavu walikuwa wanahitaji elimu maalum kwa ajili ya kuhakikisha wanajikinga na ugonjwa huo kwa kuwa kundi hilo halijawahi kukumbukwa na walikuwa hatarini zaidi kupata maambukizi hayo.

Maketa alisema kuwa kundi hilo limekuwa likisahaulika mara kwa mara kupata elimu ya magonjwa ya milipuko kuliko makundi mengine yote hivyo serikali na wadau wengine wanapaswa kujitolea kutoa elimu kwa walemavu hao.

Alisema kuwa kunapotokea milipuko ya magonjwa kama kipindupindu,homa ya matumbo na Corana wanakuwa hawapata elimu hiyo kwa wakati na kushindwa kupata mbinu sahihi za kujikinga na magonjwa hayo.

Maketa alisema kuwa watu wenye ulemavu hawaoni mambo yanayoendelea kutokana wao kuweza kusikia tu hivyo ikitolewa elimu mara kwa mara itasaidia kundi hilo kuepukana kukumbwa na magonjwa hayo ya milipuko.

Aidha kwa upande wake Mwenyekiti TLB Manispaa ya Iringa David Mgimwa alisema kuwa walikuwa wanakukumbana na unyanyapaa kutoka kwa watu waliokuwa wakiwasaidia kuwaongoza barabarani kukataa kuwashika mkono wakati wa kipindi cha Corona kwa hofu ya kupata maambukizi hayo.

Mgimwa alisema kuwa wananchi wanatakiwa kutoa ushirikiano kwa watu wenye ulemavu ili kuwasaidia kuepukana na kujikinga na magonjwa ya milipuko ambayo yanayokuwa yanatokea mara kwa mara bila watu wenye ulemavu kujua nini kinaendelea wala kutokujua namna ya kujikinga na magonjwa hayo.

Mgimwa aliwaomba wananchi kuendelea kuwasaidia na kutoa elimu kwa watu wenye ulemavu wa macho pale yanapotokea magonjwa ya milipuko ili kuwasaidia walemavu hao kujikinga kupata magonjwa hayo ya milipuko.

Lakini pia jamii imeshauriwa kuwashika mkono watu wenye ulemavu wa macho hasa katika kipindi cha mapambano dhidi ya kuenea kwa virusi vya Corona COVID 19 kwani wamekuwa wakikabiliana na changamoto mbalimbali kutokana na hali zao.

Akizungumza na mwandishi wetu mganga mkuu wa Manispaa ya Iringa, Dk. Jesca Leba alisema kwamba kutokana na hali walizonazo walemavu wa macho kuna umuhimu mkubwa wa jamii kuwa nao sambamba kwani wako katika hali ya hatari zaidi kutokana na hali zao za kutokuona hivyo elimu na kuwaongoza namna ya kunawa mikono itasaidia katika mapambano hayo.

Alisema kuwa kama manispaa wametoa mafunzo kwa walemavu na wataendelea kutoa mafunzo kwa makundi mbalimbali ya walemavu kwa ajili ya kushikwa mkono kwani changamoto kubwa kwenye vyombo vya kunawia mikono wanashindwa kuelewa mahali ilipo.

“Kwa kweli kuna changamoto kubwa kwa walemavu na ndio maana tumeamua kufanya mafunzo kwao tena maalum kwa kundi la walemavu wa macho na tutafanya mafunzo haya kwa makundi yote kwa sababu watu wanaohitaji kushikwa mikono katika kuwaongoza” alisema

Aidha katika mafunzo hayo, Dk Leba aliwataka walemavu wa macho kuepuka kushika macho, pua na mdomo kwa mikono isiyo safi kwa sababu mikono ni rahisi kubeba vimelea vya maradhi na kuzingatia ustaarabu wa kuzuia pua na mdomo wakati wa kukohoa au kupiga chafya.

Alisema kuwa endapo binaamu atahisi kuwa na mafua makali, homa, kikohozi na kushindwa kuhema nenda hospitali kupata msaada wa kitaalamu na kuepuka kuwa sehemu yenye msongamano kama vyombo vya usafiri, maduka na maeneo yenye mgandamizo wa hewa.