WATOTO wawili wa kiume wa Rais Donald Trump wamewatupia lawama wanachama wa Republican kwa kutomuunga mkono baba yao anayekabiliwa na ushindani mkali kutetea mhula wa pili madarakani.

Mtoto  mkubwa waTrump,  Don Jr amekikosoa chama hicho  kwa kuwa "dhaifu". Ndugu yake Eric ameonya: "Wapiga kura wetu hawatawahi kuwasahau mkijifanya wanyonge!"

Hatua hiyo inaasharia  mgawanyiko ulioibuka kati ya washirika wa Trump ndani ya chama.

Ushandani mkali umeshuhudiwa lakini mgombea wa Democratic Joe Biden anaonekana kuelekea kupata ushindi.

Bwana Trump ameapa kupinga matokeo ya uchaguzi huo mahakamani akitilia shaka shughuli ya kuhesabu kura inavyoendeshwa akidai kumekuwa na visa vingi vya udanganyifu.

Wanasiasa wa ngazi ya juu katika chama cha Republican kama vile seneta wa Utah Mitt Romney na Gavana wa Maryland Larry Hogan wameonya hatua ya kuhujumu mchakato wa kidemokrasia.

Lakini Don Jr, ambaye anaaminiwa kuwa na ndoto ya kujiunga na siasa ameelekeza ghadhabu yake kwa wale walio na azma ya kuwania urais mwaka 2024.

Aliandika kwenye Twitter: "Hatua ya kutochukua hatua kwa wanasiasa 'wanaotaka tiketi ya 2024 ya [Republican] ' inashangaza sana .

"Wana nafasi ya kuonesha kutoridhishwa kwao na hali ilivyo na kupigania wanachokiamini lakini wanahofia kuangaziwa vibaya na vyombo vya habari. Msiwe na hofi @realDonaldTrump ataendelea kupambana na wao wakiangalia!"

Ujumbe huo wa Twitter hiyo ulikuwa unamjibu Mike Cernovich, mwanaharakati wa masuala ya wanaume na mfuasi wa Trump, ambaye alikuwa amemkosoa mjumbe maalum wa zamani wa rais katika Umoja wa Mataifa , Nikki Haley.

Anadhaniwa na wengi kwamba anapania kuingia Ikulu ya White House mwaka 2024.

Bwana Trump Jr aliendelea kuandika: "Republicans wamekuwa wanyonge kwa miongo kadhaa hali iliyotoa nafasi kwa wapinzani kufanya vitu hivi."

Ndugu yake Eric, aliandika: "Sisi ni Warepublican! Tuna ubavu wa kukabiliana na udanganyifu. Wapiga kura wetu hawatawahi kusahau mlichokifanya!"

-BBC