Mkuu wa mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila, amesema kuwa asilimia kubwa ya wanawake wa mkoa wa Mbeya, wameachiwa jukumu la kuendesha familia zao huku wanaume wakiongoza kufanya vitendo vya dhuluma dhidi ya mali zinazotafutwa na wake zao.


Chalamila ameyasema hayo wakati akifunga kongamano la sita la jinsia ngazi ya wilaya, ambalo limefanyika katika Halmashauri ya wilaya ya Mbeya.


RC Chalamila amesema kuwa wanawake wengi mkoani humo, ndiyo wanaobeba majukumu ya kutunza na kulea familia, ambapo hufanya shughuli mbalimbali za ujasiriamali ikiwemo kuuza mboga na matunda, wakati wanaume wakitumia mwanya huo kuwafanyia vitendo vya ukatili wa kijinsia ikiwa ni  pamoja na kunyang'anya fedha wanazopata kwenye biashara na kwenda kuhonga michepuko.


"Idadi kubwa ya wanaume mkoani Mbeya, wanapenda kulelewa hawapendi kujishughulisha, wanawategemea wanawake kulisha familia na kufanya kila kitu, mbaya zaidi huwashinikiza wake zao kuomba mkopo kwa kutumia account zao ili wadhulumu hizo hela, nawaambia wanawake msikubali kutumika kama ndoa yako ina shida  ondoka kaanzishe maisha mengine", amesema RC Chalamila.