Maandamano ya wafuasi wa rais wa Marekani, Donald Trump mjini Washington DC yameingia kwenye machafuko baada ya kuzuka mapigano baina yao na watu wanaopinga ubaguzi wa rangi.

Televisheni ya Russia Today imeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, wafuasi wa Donald Trump wamefanya maandamano wakidai kuibiwa kura na walielekea kwenye jengo la Mahakama Kuu ya mji huo. 

Wafuasi wa magenge ya mirengo ya kulia yenye misimamo mikali ambao mengi wao walikuwa na silaha, wameshiriki kwenye maandamano hayo. 

Waandamanaji hao wamepigana na kundi moja la Wamarekani wenye asili ya Afrika ambao nao walikuwa wamekusanyika kumpinga Donald Trump. 

Jeshi la polisi lililazimika kuingilia kati kuzima mapigano hayo. Rais huyo wa Marekani alijitokeza mbele ya wafuasi wake katika maandamano hayo ili kuwaunga mkono.

Mara kadhaa Trump amekuwa akisema kwamba mfumo wa uchaguzi wa Marekani ni mbovu na mharibifu kupindukia. Msemaji wa White House, Kayleigh McEnany, amedai kuwa zaidi ya wafuasi milioni moja wa Trump wameshiriki kwenye maandamano hayo. 

Hata hivyo picha za vyombo vya habari zinaonesha kulikuwa na watu  elfu kadhaa tu ya wafuasi wa Trump katika maandamano hayo. 

Licha ya takwimu za vyombo vya habari vya Marekani kuonesha kuwa, Donald Trump ameshindwa katika uchaguzi wa rais wa Novemba 3, 2020, lakini bado rais huyo anang'ang'ania kuwa yeye ndiye mshindi. Amefungua mashtaka mahakamani kulalamikia uchaguzi huo.