NA TIGANYA VINCENT
UONGOZI wa Mkoa wa Tabora umekutana na wafanyabiashara wa vifaa vya ujenzi na saruji na kukubaliana faida wanayopata katika kila mfuko mmoja wanayouza isizidi shilingi 500/= baada ya kuondoa gharama mbalimbali wazizotumia ili kutowaumizi wananchi wanyonge.

Wamefikia uamuzi huo  katika Mkutano ambao uliongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Tabora Dkt.Philemon Sengati kwa lengo la kutafuta muafaka wa kutatua tatizo la bei ya saruji kupanda.

Akifungua mkutano huo Mkuu wa Mkoa alisema Serikali haikusudi kuwapanga bei elekezi ya saruji lakini wafanyabiashara wanalojukumu la kuuza bidhaa hiyo kwa bei ambayo haitawafanya wananchi wanyonge washindwe kujenga na kuishi katika nyumba bora.

Dkt. Sengati alisema kimsingi hakuna sababu ambazo zinazoweza kuhalalisha wafanyabiashara hao kupandisha saruji ambapo wapo wanauza shilingi 23,000/- hadi 30,000/= kwa mfuko mmoja wakati wao wananua kiwandani kwa wastani unaoanzia 11,000 hadi shilingi 13,000/=.

Alisema gharama za usafirishaji na posho za vibarua na madereva haiwezi kufanya bei ipande kwa kiasi hicho ambacho inawaumiza wananchi.

Dkt. Sengati alisema pamoja na kuwa sio jukumu la Serikali kupanga bei lakini ina wajibu wa kuhakikisha bei za bidhaa zilizoko sokoni haziwaumizi wananchi wanyonge na kuwafanya wachukie Serikali yao

Alisema wafanyabiashara ni wadau muhimu katika kushirikiana na Serikali kwenye shughuli za maendeleo ni vema wakahakikisha saruji inauzwa kwa bei nafuu ambayo haiwaumizi wananchi na kuwafanya wajisichie Serikali yao.

“Tumebaini wafanyabiashara wa rejareja wanauza saruji kwa shilingi 23,000/= hadi 30,000/= wakati bidhaa hizo amechukulia hapa hapa Tabora na hana gharama kubwa za kusafirisha mizigo…kitendo hicho ni kutaka kutengeneza fedha nyingi kwa kuwaumiza wanyonge… hakikubaliki, serikali haiwezi kuvulimia ,tutawachukulia hatua” alisema.

Dkt. Sengati alisema wafanyabiashara wanatakiwa kuwa wazalendo kwa kuungana na maono na mtazamo wa Serikali ya Awamu ya Tano ambao unataka ubora na unafuu wa maisha kwa wananchi.

Mmiliki wa Kampuni ya Vimajo and Sons ambaye ni miongoni  wa wanyabishara wakubwa wa Saruji Mkoani Victor Chami alisema hivi sasa saruji inapatikana kwa shida na wakati mwingine wanalazimika kununua kwa wafanyabiashara wenzao ambao wanaakiba  na ndio maana ameongeza kiashi hicho kidogo.

Mfanyabiashara huyo aliongeza kuwa hivi sasa wameamua kununua saruji aina ya Camel baada ya waliyokuwa wakinunua kwa wingi Mkoani Tabora ya Dangote kutopatikana.

Alisema wananunua saruji hiyo kwa gharama ya shilingi 13, 340/= kiwandani Dar salaam na  gharama za usafiri ni shilingi 5,000/= na vibarua wa kushusha wanawalipa shilingi 100/= na zinazobaki ndio faida yao.

Chami alisema kutoka na uhitaji mkubwa wa saruji hapa nchini kwa sababu ya miradi mikubwa inayojengwa na Serikali na mahitaji ya wananchi ni vema Seikali ikawabana Wazalishaji wa Saruji ili waongeza uzalishaji na waachane na kupeleka nje ya nchi.

Alisema pindi Serikali itakapokamilisha miradi yake ndio wazalishaji waruhusiwe kupeleka nje ya Tanzania.

Chami alisema yeye atauza saruji kwa bei ya awali ya shilingi 18,500/= kama ilivyokuwa kabla ya kuadimika kwa saruji mkoani humo.

Naye Beatus Massawe alisema ili kukabiliana na tatizo la uhaba wa saruji mkoani ni vema kumuomba Dangote kuanzisha Ghala kubwa Tabora kwa ajili ya Mikoa ya Kanda ya Magharibi.

Alisema kuwepo kwa ghala hilo litawasaidia kupata bidhaa hiyo kwa muda mfupi na gharama ambayo itawafanya wauze kwa bei ya chini kwa wananchi.

Massawe alisema sanjari na hilo alimuomba Mkuu huyo wa Mkoa wa Tabora ili awasiliane na Shirika la Reli Tanzania liweze kuongeza Mabehewa ya kuleta saruji kwa wingi mkoani Tabora.

Baada ya mkutano huo Wafanyabiashara hao kwa pamoja walikubaliana kuwa bei ya Saruji aina ya Simba kwa rejareja iuzwe kwa shilingi 18,500/- kwa mfuko, Dangote iuzwe kwa kiwango cha shilingi 19,000/=, Camel iuzwe kwa shilingi 19,500/= na Nyati iuzwe kwa shilingi 20,000/-.
Walifikia uamuzi huo baada ya kujumulisha gharama kutoka uzalishaji kiwandani , za usafiri, posho ya vibarua na faida ya Mawakala.
Mkuu wa Mkoa wa Tabora alisema baada ya makubaliano hayo Serikali haitasita kuwachukulia hatua wafanyabiashara ambao watakutwa wanauza zaidia ya hapo.