Na Omary Mngindo, Mkuranga.

JUMUIA ya Umoja wa Vijana ndani ya Chama Cha Mapinduzi UVCCM Wilaya ya Mkuranga Mkoa wa Pwani, imempongeza Waziri na Manaibu Waziri wawili wanaotokea mkoani hapa.

Mbunge wa Jimbo la Kisarawe Suleiman Jafo (Waziri wa TAMISEMI) wa Mkuranga Abdallah Ulega (Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi) na wa Viti Maalumu Subira Mgalu (Naibu Waziri wa Nishati) ambao wamehudumia Wizara hizo kipindi kinachomalizika.

Pongezi hizo zimetolewa na Katibu wa Jumuia hiyo wilayani hapa Hanzuruni Mtebwa, akizungumza na Waandishi wa habari wilayani Mkuranga, mbapo alisema Mawaziri hao wamezitendea haki Wizara zao, jambo ambalo ni la kujivunia kwa wana-Pwani.

"Wana-Pwani tuna kila sababu ya kutembea kifua mbele, hii imetokana na Wabunge wetu walioteuliwa na Rais wetu mpendwa Dkt. John Magufuli, kuziongoza Wizara hizo, ambao kiukweli hawakumuangusha Rais, UVCCM Mkuranga tunawapongeza sana," alisema Mtebwa.

Alisema kuwa Rais Magufuli alipowateua Mawaziri hao hakuna aliyedhani kwamba wangeweza kuzitumikia Wizara hizo, hususani ya TAMISEMI ambayo katika vipindi vilivyopita Mawaziri wengi walioteuliwa walikuwa wanaishia njiani, kwa maana ya kushindwa kuzitumikia ipasavyo.

"Hakika Rais Magufuli alituheshimisha wana-Pwani, nao wameweza kuzitendea haki nafasi hizo tunatembea kifua mbele kutokana na namna walivyozitendea haki Wizara husika, kwani kazi tumeziona wametekeleza majukumu yeo kiuhakika," alisema Katibu huyo.

Aliongeza kwamba hatua ya uteuzi wao imetosha kuwa kielelezo cha uadilifu waliokuwanao kabla, na hiyo imethibitisha baada ya kuzitendea haki nafasi hizo, na kwa namna walivyozimudu kwani kipindi chote hakukuwepo malalamiko kuhusiana na utendaji wao.

"Hatukuwahi kusikia minong'ono yenye ukakasi iliyoelekezwa kwao wakati wa kuwahudumia wananchi, wameweza kuendana na kasi ya Rais na hitajio la wa-Tanzania na nafasi zao kwani hawakumuangusha aliyewateuwa, tunawashukuru sana," alisema Katibu huyo.

Alisema kwamba huduma zao zilizotokana na uteuzi wa awali, imekuwa mbegu njema iliyodhihirishwa kwenye kura za maoni, sanjali na ushindi wa kishindo katika uchaguzi Mkuu wa Oktoba 28 hivyo kudhihirisha kwamba jamii bado inawahitaji.

"Niwaombe waendelee kuwa wahudumu  wananchi kama ilivyo desturi yao, imani yetu ni kwamba kutokana na Rais Magufuli kupenda viongozi wachapakazi kwa mapenzi ya Mwenyeezimungu wanaweza kurejea katika nafasi zao," alisema Mtebwa.

Katibu huyo alimalizia kwa kuwashukuru wote ambao kwa namna moja ama nyingine, walitambua mchango wao katika kuhudumu na kuona wanafaa kuchaguliwa tena kuwa wabunge katika maeneo yao ya Ubunge.