Mjini kuna mambo! Wikiendi iliyopita kulisambaa tetesi kwamba mjengo wa kifahari anaoishi msanii wa muziki wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ uliopo Mbezi-Beach jijini Dar, upo mbioni kuuzwa, Gazeti la IJUMAA WIKIENDA limechimba ishu hiyo na kuibuka na ukweli wake.

Ishu hiyo ilianza kusambaa kwenye mitandao ya kijamii ambapo ilidaiwa kwamba, mmiliki wa mjengo huo anayefahamika kwa jina moja la Lazaro, yupo mbioni kuuza mjengo huo kwa kiasi cha shilingi bilioni 1.4.

Gazeti la IJUMAA WIKIENDA lilizungumza na mmoja wa watoa habari ambaye alidai kuwa, Lazaro anauza nyumba hiyo anayoishi Mondi kwa sababu msanii huyo ameshindwa kuinunua. “Mimi nimeona hiyo nyumba kabisa, tena mwenye nyumba ameweka mpaka tangazo nje anaiuza, sasa mnaweza kufuatilia ili kujua ukweli upo vipi,” kilisema chanzo hicho.

WIKIENDA MZIGONI…

Ili kujiridhisha, Gazeti la IJUMAA WIKIENDA lilitinga nyumbani kwa Mondi asubuhi na mapema ambapo baada ya kufika eneo hilo, halikuona bango linaloonesha mjengo huo kuuzwa na hata baada ya kuongea na baadhi ya majirani, nao walikuwa na haya ya kusema;

“Mmmh! Hapana kwa kweli kwa sababu huu mjengo ungekuwa unauzwa sisi tungepata taarifa na hata hilo bango la tangazo wanalosema limewekwa nje mbona halipo au wewe (anamuuliza mwandishi) umeliona?

“Unajua kuna kipindi tulisikia kwamba Diamond alimuomba Lazaro amuuzie huu mjengo, lakini wakashindwana bei kwa sababu mwenye nyumba alikuwa anataka pesa nyingi sana, hivyo ikambidi Mondi aahirishe tu,” alisema jirani huyo

UONGOZI WA MTAA WANENA

Gazeti la IJUMAA WIKIENDA pia lilizungumza na mmoja wa viongozi wa mtaa huo anaoishi Mondi, Nassoro Mgaywa ambaye kwa upande wake alisema kuwa, hana taarifa za mjengo huo kuuzwa na kama ingekuwa ni kweli, basi angefahamu.

“Kiukweli sina taarifa zozote za kuuzwa hii nyumba, mwenye nyumba ni mtu wa karibu sana na mimi, hivyo kama kweli angekuwa anauza, lazima angetujulisha sisi viongozi wake wa Serikali ya mtaa,” alisema Nassoro.

KUMBE NI MJENGO MWINGINE…

Baada ya kujiridhisha, Gazeti la IJUMAA WIKIENDA lilipata taarifa kutoka kwa dalali maarufu mjini wa kuwapangishia nyumba mastaa anayejulikana kwa jina la Dalali Kiongozi ambaye alisema kuwa, ni kweli mwenye nyumba anauza mjengo wake, lakini siyo huo anaoishi Mondi

“Yule baba (Lazaro) ana nyumba nyingi sana, hiyo nyumba anayoiuza ipo Mbweni (Dar), ila imefanana kila kitu na hii anayoishi Diamond hapa Mbezi-Beach hivyo baada ya watu kuiona mtandaoni, nadhani wakajua ni hii kwa sababu inafahamika kumbe siyo,” alisema Dalali Kiongozi.

Taarifa zilizopo ni kwamba, kwenye nyumba hiyo Mondi ni mpangaji ambapo kodi inalipwa na kampuni moja ya vinywaji ambayo yeye ni balozi wake.


Stori: Memorise Richard, Dar