Aliyekuwa mgombea wa urais wa chama cha upinzani cha Chadema Tundu Lissu ameondoka Tanzania leo Jumanne Novemba 10,2020 kwenda Ubeligiji.
Lissu amesafiri akiwa anatokea katika makazi ya Balozi wa Ujerumani nchini Tanzania ambako aliomba hifadhi wiki iliyopita akidai kutishiwa maisha yake.
Lissu ametuma video fupi kupitia mtandao wake wa Twitter ikionesha akitoka kwenye nyumba ya balozi mpaka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere alipopanda ndege na kuelekea Ubelgiji mchana wa leo.
— Tundu Antiphas Lissu (@TunduALissu) November 10, 2020
Mwisho wa Twitter ujumbe, 1
Kwa mujibu wa gazeti la Mwananchi, Lissu alisindikizwa na maafisa wa ubalozi wa Ujerumani na Marekani katika safari yake hiyo.
Lissu alikuwa akiishi nchini Ubelgiji toka Januari 2018 wakati akipata matibabu baada ya kushambuliwa vibaya kwa risasi na watu wasiojulikana Septemba 2017 Dodoma, Tanzania.
Mwanasiasa huyo alirejea Tanzania mwezi Julai mwaka huu ili kuwania nafasi ya urais ambapo alishindwa na rais John Magufuli wa chama tawala CCM.
Lissu na chama chake wakishirikiana na ACT-Wazalendo walikataa kukubali matokeo hayo na kuitisha maandamano ambayo hata hivyo hayakufanyika na baadhi ya viongozi wa vyama hivyo kukamatwa kwa muda. Mara baada ya kuachiwa, Novemba 2, Lissu aliomba hifadhi kwa Balozi wa Ujerumani akisema amepokea vitisho juu ya maisha yake.
Lissu anakuwa mwanasiasa wa pili mkubwa wa upinzani kuondoka Tanzania baada ya uchaguzi, wa kwanza akiwa aliyekuwa mbunge wa Arusha Mjini Godbless Lema ambaye amepewa hifadhi wiki hii nchini Kenya. Lema pia ametaja vitisho vya usalama kama sababu ya kuondoka Tanzania.
Hata hivyo msemaji wa serikali ya nchi hiyo Dkt Hassan Abbas amekanusha kuwa kuna vitisho kwa wanasiasa wa upinzani nchini humo.
The post Tundu Lissu aondoka Tanzania na kurejea Ubelgiji (+Video) appeared first on Bongo5.com.