Imefahamika kwamba Rais Donald Trump wa Marekani alikaribia sana kuchukuwa maamuzi ya kuvishambulia vinu vya nyuklia vya Iran miezi miwili tu kabla ya kuondoka madarakani.

Taarifa ya uchunguzi iliyochapishwa jana (Jumatatu, 16 Novemba) na gazeti la New York Times inasema kwamba Trump aliwauliza wasaidizi wake wakuu juu ya uwezekano wa kuvishambulia vinu vya nyuklia vya Iran siku ya Alhamis iliyopita.

Kwa mujibu wa shirika la habari la AFP, kwenye mkutano wake na Makamu wa Rais Mike Pence, Waziri wa Mambo ya Kigeni Mike Pompeo na Mkuu wa Majeshi Jenerali Mark Milley, Trump alitaka kujuwa endapo kuna njia yoyote anayoweza kutumia kuchukuwa hatua dhidi ya maeneo yanayoaminika kuwa na vinu vya nyuklia nchini Iran ndani ya wiki chache kutoka sasa.

Hata hivyo, gazeti la  New York Times linasema kwamba wasaidizi hao wa Trump walimshauri kutokuchukuwa hatua ya kijeshi, wakimuonya kuwa "mashambulizi kama hayo yanaweza kugeuka kuwa mzozo mkubwa" kwenye wiki hizi za mwisho za urais wake.

Sababu ya Trump kuulizia uwezekano huo wa kuishambulia Iran inatajwa kuwa ni ripoti ya Shirika la Nguvu za Atomiki Duniani (IAEA) iliyosema kwamba Iran inaendelea na kukusanya madini ya uranium yanayotumika kutengenezea silaha za nyuklia.

Uchunguzi wa New York Times umebainisha kwamba maeneo ambayo yangeliweza kushambuliwa na Marekani ni pamoja na Natanz, ambako IAEA inasema kuwa kiwango cha madini ya uranium cha Iran sasa kimeongezeka mara 12 zaidi ya kile kinachoruhusiwa na mkataba wa nyuklia ambao Trump alijiondowa mwaka 2018.

 

Credit:DW