Donald Trump alisisitiza kuwa hakubaliani na matokeo ya uchaguzi wa Marekani, lakini ameonekana kukubali matokeo kwa mara ya kwanza kuwa mpinzani wake wa Democrat Joe Biden ameshinda."Ameshinda uchaguzi kwa kuwa mchakato wa uchaguzi ulikuwa wa wizi," ameandika kwenye kurasa yake ya Twitter lakini baada ya dakika chache alisema hamaanishi kuwa alishindwa uchaguzi wa Novemba 3.
Bwana Trump alirudia tena madai yake ya kuibiwa katika uchaguzi.
Alifungua kesi kuhusu madai yake lakini hakutoa ushaidi wowote wa madai hayo ya kuibiwa.
Mashtaka yake yote yamepuuziwa.
Ijumaa, maafisa wa uchaguzi walisema uchaguzi wa mwaka huu ulifanyika katika usalama zaidi katika historia ya Marekani na hakuna ushaidi kuwa kura zilipotea au kuibiwa au kuwa na tatizo lolote la kufanya uchaguzi kutiliwa shaka au batili.
Pamoja na ufafanuzi huo , Trump hakukubali kuwa Biden alishinda uchaguzi mpaka sasa.
Ijumaa, msemaji wa Ikulu Kayleigh McEnany aliiambia Fox News: "Rais Trump anaamini kuwa atakuwa rais kwa muhula wa pili."
Katika mkutano na wanahabari siku hiyohiyo , Bwana Trump alisema "Nani anajua mamlaka ipi itakuwa madarakani siku zijazo".
Licha ya kukubali ushindi wa Biden katika ujumbe mmoja wa tweet Jumapili hii, rais aliongeza kusema "Sikubaliani na LOLOTE!".
Twitter iliongeza tahadhari kwa Trump kuhusu madai yake na kusema "Madai ya kuibiwa katika uchaguzi yanapingwa".
Maelfu ya wafuasi wa wa Trump waliandamana Washington DC Jumamosi kupinga madai yao kufutwa.
Maandamano ya amani yalikumbwa na vurugu majira ya jioni baada ya wafuasi hao kuanza kufanya fujo.
Maofisa walisema watu 20 wameshtakiwa kwa makosa mbalimbali yakiwemo ya kushambulia watu na umiliki wa silaha.
Tukio moja la mtu kuchomwa kisu liliripotiwa na polisi wawili kujeruhiwa.
Kwa sasa kuna msukumo mkubwa kwa Trump kujiandaa kukabidhi mamlaka kwa amani.
Wakala wa huduma ya uongozi (GSA)wakala wa serikali wanajukumu la kuanza mchakato wa kuwatambua Biden na makamu wake Kamala Harris kuwa washindi.