Na Mwandishi wetu- Arusha
Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limeteketeza vipodozi  vyenye viambata sumu  vya thamani ya Shilingi milioni 125 baada ya  kufanyika kwa ukaguzi wa kushitukiza kwenye maghala ya kuhifadhia vipodozi ambayo hayajasajiliwa.


Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa mwishoni mwa wiki na TBS, Vipodozi hivyo vilivyopigwa marufuku vilikutwa katika maghala la kampuni ya Kimario Cosmetics  hivi karibuni na wakaguzi wa TBS  Jijinii Arusha na kukamatwa  kwa mujibu wa Sheria ya Viwango Na. 2 ya mwaka 2009 pamoja na Marekebisho yake ya Mwaka 2019.


“Mmiliki wa ghala hilo Pamphil L. Kimario amelipa shilingi milioni 3.5 ikiwa ni gharama ya kuteketeza  bidhaa hizo  hatarishi kwa afya ya binadamu  kwani zinapotumiwa huweza kusababisha  madhara mbambali kwa mtumiaji”,Inasisitiza taarifa hiyo


Taarifa hiyo imeeleza kuwa, Baadhi wa Watanzania wamekuwa wakitumia vipodozi hivyo vyenye viambata vya sumu ambavyo vina kemikali ya Mercury na Hydoroquinone kwa lengo la kung’arisha  ngozi zao  na hata kubadili rangi ya ngozi hizo bila kujali madhara yatokanayo na bidhaa hizo.


Vipodozi vyenye kemikali ya Mercury kwa Mujibu ripoti ya Shirika la Afya Duniani(WHO) ya mwaka 2020, vikitumika kwa muda mrefu vinasababisha magonjwa ya figo, mapafu, ngozi, macho mfumo wa fahamu mfumo wa mmeng’enyo wa chakula na mfumo  wa  kinga ya mwili na kwa upande wa matumizi ya vipodozi vyenye kemikali ya hydroquinone husababisha magonjwa ya kansa ya ngozi.


Aidha, Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Sheria ya Fedha  Na. 8 ya mwaka 2019 iliipa Mamlaka TBS  ya kusimamia usajili wa bidhaa za chakula ,vipodozi , maghala ya kuhifadhia chakula na vipodozi pamoja na migahawa na mahoteli jukumu  lillilokuwa likifanywa hapo awali na iliyokuwa Mamlaka ya Dawa Chakula na Vipodozi (TFDA).


Utekelezaji wa Sheria hiyo ya Fedha ulianza rasmi tangu Julai 2019, hivyo kuwalazimu wauzaji wazalishaji  na wauzaji wa vipodozi kusajili bidhaa hizo pamoja na  maghala ya kuhifadhia.


Shirika pia limeteketeza bidhaa nyingine zisizofaa za vipodozi na vyakula  zilizokamatwa katika kaguzi zilizofanyika nyakati tofauti  katika maeneo mengine Arusha na nje ya Arusha  katika kipindi cha Januari  hadi  Novemba 2020.  


TBS inaendelea na ukaguzi huu nchi nzima  pamoja na kuwahimiza wazalishaji na wauzaji wa vipodozi kuhakikisha kuwa wanafuata taratibu zilizopo kwa kusajili bidhaa hizo pamoja na maghala  ili kuepuka usumbufu. Pia wauzaji wa vipodozi wanahimizwa kuwa na orodha ya bidhaa za vipodozi visivyoruhusiwa ambayo inapatikana katika tovuti ya Shirika https://bit.ly/335vgov