Timu ya Taifa ya Wasichana ya Tanzania chini ya umri wa miaka 17 ‘Tanzanite Queens’ imefanikiwa kutwaa ubingwa wa michuano ya COSAFA kwa upande wa Wanawake baada ya kupata ushindi kwa penalti 4-3 dhidi ya wapinzani wao Zambia katika mchezo wa fainali uliochezwa kwenye dimba la Nelson Mandela Bay baada ya 90 kumalizika kwa sare ya bao 1-1.

Zambia walikuwa wa kwanza kupata goli lililofungwa dakika ya 19 na mshambuliaji Comfort Seleman ambaye alitumia vizuri makosa ya safu ya ulinzi ya Tanzania baada ya kuondoka na mpira kuanzia katikati ya uwanja hadi kwenye goli na kupiga shuti ambalo lilimsinda golikipa Aisha Mrisho.

Lakini kipindi cha pili Tanzania ilisawazisha bao hilo kwa mkwaju wa penalti iliyopigwa na Koku Kipanga baada ya Aisha Masaka kuchezewa madhambi ndani ya eneo la 18 na mchezo huo kumalizika kwa sare ya goli 1-1.

Ushindi huo sasa umewahakikishia timu hiyo kubeba kitita cha dola za Kimarekani 15,000 ambazo ni zaidi ya Sh. milioni 34 walizoahidiwa na Kamati ya Saidia Ushindi ya Taifa Stars ikiwa watatwaa ubingwa huo.