Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeihibitishia jumuiya ya kimataifa kuwa itaendelea kutoa vikosi vya kulinda amani na ulinzi katika nchi za bara la Afrika.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) wakati alipokuwa katika mkutano wa kunzindua kikosi kazi cha kuandaa Mpango Kazi wa Kitaifa juu ya wanawake, amani na usalama jijini Dar es Salaam.

Prof. Kabudi amesema kuwa serikali ya Tanzania ipo tayari kufanya kazi kwa kushirikiana na Shirika la Mwalimu Nyerere na Shirika la Umoja wa Mataifa pamoja na mashirika mengine duniani katika kuhakikisha kuwa amani ulinzi na usalama vinapatikana.

"Tanzania imekuwa ni nchi mojawapo inayotoa askari wanaokwenda kulinda amani katika mataifa mbalimbali katika bara la Afrika ambapo baadhi yake ni Sudani, Congo DRC, Lebanon na Afrika ya Kati……… kwa hiyo lengo la mpango kazi huu ni kuwezasha Serikali ya Tanzania kuboresha ushiriki wa askari wa kike katika masuala ya ulinzi na amani," Amesema Prof. kabudi

Aidha, Prof. Kabudi ameeleza kuwa Tanzania itaendelea kutoa askari wa kulinda amani katika mataifa mbalimbali barani afrika kwani suala la amani katika jamii ni jambo muhimu sana kwa maendeleo ya Taifa lolote lile Duniani.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku, amesema kuwa Taasisi anayoiongoza iko tayari kufanya kazi kwa karibu na jumuiya ya kimataifa na washirika wote wa maendeleo katika kuhakikisha kuwa amani na utu wa mwanamke unalindwa na kuheshimiwa katika jamii.

Pamoja na mambo mengine, mkutano huo pia ulihudhuriwa na mabalozi mbalimbali wanaowakilisha nchi zao hapa nchini, akiwemo Balozi wa Norway, Mhe. Elisabeth Jacobsen, Balozi wa Nchi za Falme za Kiarabu, mhe. Khalifa Abdulrahman Mohammed Ali-Marzouki, Balozi wa Canada Mhe. Pamela O'Donnell pamoja Mratibu Mkazi wa Shughuli za Umoja wa Mataifa (UN) Bw. Zlatan Milišić.