Mkurugenzi mkuu Takukuru, Brigedia John Mbungo amesema ofisi yake kwa kushirikiana na mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Zipora Liana wamedhibiti Sh12 bilioni ambazo zingelipwa kinyume na mipango katika mradi wa ujenzi wa stendi mpya ya mabasi mkoa wa Dar es Salaam.

Mbungo ameeleza hayo leo Jumamosi Novemba 14, 2020 katika mkutano wake na waandishi wa habari.

Amesema fedha hizo zilikuwa zinalipwa kwa makandarasi kama ziada kwa kazi ambayo haikufanyika.

"Udhibiti huu umefanikiwa kwa kuwa na wachunguzi na wataalamu wa ujenzi kutoka Takukuru waliokuwa wakifuatilia kazi hii kwa karibu,” amesema.

Mbungo ametoa pongezi kwa  Liana huku akitoa wito kwa wakurugenzi wengine kuendelea kushirikisha na taasisi hiyo kufuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo ili kuhakikisha fedha za Serikali zinazotokana na kodi za wananchi zinatumika kulingana na malengo yaliyowekwa.