Aliyekuwa mbunge wa jimbo la Mbeya Mjini, (CHADEMA), Joseph Mbilinyi, amemtaka Mbunge wa Sasa Wa jimbo hilo Dkt Tulia Ackson kufuata utaratibu ili apewe ofisi ya Jimbo badala ya kumlalamikia yeye, kwani yeye hana mamlaka ya kumkabidhi ofisi mbunge.

Sugu amesema ofisi aliyokuwa akiitumia kama Mbunge ambayo alipewa na Halmashauri, alikwisharudisha funguo kwa mamlaka husika na kwamba aachane nae na achape kazi.

Siku ya Jumatatu ya Novemba 23, mwaka huu mbunge mpya wa jimbo hilo wakati akizungumza na wanahabari nyumbani kwake, jijini Mbeya, alilalamika kuwa bado hajakabidhiwa ofisi aliyokuwa akiitumia mbunge Sugu na kwamba ataendelea na majukumu yake hawezi kumngoja kwani mlolongo ni mrefu.

Kauli hiyo ya Sugu ameitoa hii leo Novemba 26, 2020, wakati akizungumza na kituo cha habari cha EATV, na kuongeza kuwa hata yeye wakati anaingia kwenye hiyo ofisi zilizopo kwenye ofisi za ardhi, alikabidhiwa na halmashauri ya jiji na si yule mbunge aliyekuwepo kabla yake.

"Wewe umeshasikia wapi mbunge analia hajakabidhiwa ofisi, hakuna kitu kama hicho, aliyempa cheti cha ubunge ndiye angemwelekeza kwamba kinachofuata ni nini, afanye kazi aachane na Sugu", amesema Sugu.

Aidha Sugu ameongeza kuwa, "Yeye afuate utaratibu pengine hata sasa wamempa ofisi nyingine yeye ni mtu wa kujimwambafai, labda ofisi niliyokuwa naitumia mimi ni ndogo nadhani haitaki anatafuta 'justification' wampe ofisi kubwa zaidi kwa kusema Sugu hajanikabidhi ofisi, ofisi ni mali ya jiji" - amesema Sugu.