Winga machachari Mtanzania, Simon Msuva, amethibitisha kujiunga na Klabu ya Wydad Casablanca ya nchini Morocco kwa mkataba wa miaka minne na nusu akitokea Difaa El Jadida ya hukohuko huku akitaja sababu ya kutua kikosini hapo ni kutimiza ndoto zake.

Wydad ni moja ya klabu kubwa barani Afrika yenye historia kubwa ya soka la bara hili ambayo imewahi kutwaa Kombe la Shirikisho Afrika na Ligi ya Mabingwa Afrika ambayo msimu wa 2019/20 iliondolewa hatua ya nusu fainali ya michuano ya Ligi ya Mabingwa.

 Msuva amesema kuwa ameondoka Difaa kwa mapenzi yake mwenyewe kutokana na malengo aliyokuwa nayo hivi sasa ili kufikia ndoto alizonazo.

Msuva amesema kuwa kikubwa kilichompeleka huko ni maslahi mazuri aliyowekewa mezani na kingine ni ushiriki wa michuano ya kimataifa Afrika ambayo Wydad watashiriki Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu.

Aliongeza kuwa, kikubwa ni kutaka kuonekana kimataifa wakati timu hiyo ikishiriki michuano hiyo ambayo anaamini malengo na ndoto zake zitatimia.

“Kabla ya kujiunga na Wydad nilipata ofa nyingi lakini hazikuwa na maslahi mazuri kwangu, kama unavyofahamu soka ndiyo linaloendesha maisha yangu ni muhimu kuangalia maslahi kwanza.

“Yote kwa yote namshukuru Mungu, kikubwa niwaahidi Watanzania kuendelea kupambana huku nikimshirikisha yeye bila ya kukata tamaa ili kufanikisha malengo yangu,” amesema Msuva.