Mkuu wa shirika la mpango wa chakula duniani WFP ameonya kuwa huenda idadi kubwa ya watu wakakumbwa na baa la njaa mwaka ujao.

David Beasley amesema iwapo hatua za haraka hazitachukuliwa, idadi kubwa ya watu huenda wakakabaliwa na uhaba wa chakula ndani ya miezi michache ijayo.

Mkuu huyo wa shirika la mpango wa chakula duniani amesema hali huenda ikawa mbaya zaidi mwaka ujao hata kuliko mwaka huu.Hali hiyo ya uhaba wa chakula inatokea wakati huu ambapo ulimwengu unakabiliwa na janga la virusi vya Corona.

Katika mahojiano na shirika la habari la Marekani la Associated Press, Beasley amesema shirika hilo lililoshinda ya tuzo ya Nobel linatuma ujumbe kwa ulimwengu kwamba hali inazidi kuwa mbaya.

Beasley amesema shirika hilo linahitaji bilioni 15 za Kimarekani mwaka ujao ili kuendesha mipango yake ya kusambaza misaada.