SHEHE Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salim amemvaa na kumuonya staa wa Bongo Fleva, Benard Paul ‘Ben Pol’ ambaye hivi karibuni zilisambaa picha mitandaoni ikisemekana amebadili dini kutoka Ukristo na kuingia Uislam.

 

Hata hivyo, kabla ishu hiyo iliyoshtua wengi ikiwa haijapoa, ghafla kumeibuka tena madai mapya kwamba, Ben Pol hakubadili dini, isipokuwa ilikuwa ni kiki.

 

Taarifa za awali zilidai kuwa, Ben Pol alibadili dini huku zikishibishwa na picha ya cheti kilichomuonesha jamaa huyo kwa sasa ni Muislam.

 

Si cheti hicho tu, bali Ben Pol alionekana akiwa kwenye vazi la kanzu ambalo hutumiwa zaidi na na Waislam huku akiwa na watu wengine walivaa vazi hilo lenye heshima kwenye dini hiyo.

 

Kitendo hicho kilionekana kuwachanganya wengi ambapo maneno mengi yalianza kuzuka mitandaoni juu ya ndoa yake ya Kikatoliki aliyofunga miezi kadhaa iliyopita na mkewe, Anerlisa Muigai, raia wa Kenya huku wengine wakidai hapo hakuna tena ndoa.

 

Wakati hayo yakiendelea, Ben Pol ni kama alikuwa mafichoni kwa maana mapaparazi wetu walianza kumsaka kila kona ili kufanya naye mahojiano, lakini waligonga mwamba.

 

Katika harakati za kutaka kujua undani wa tukio hilo, IJUMAA lilianza kumsaka mkewe huyo (Anerlisa) ili naye aweze kuzungumzia suala hilo, lakini hakupatikana hewani ambapo baadaye taarifa zilidai alikuwa kwao nchini Kenya.

 

Juhudi hizo ziliendelea na kumfikia mama yake mzazi, Cecilia Buhondo ambaye baada ya kuulizwa kuhusu suala la mwanaye huyo kubadili dini, alionesha kupigwa na mshangao na kusema hajui chochote.

 

Mambo yakiwa hivyo, mwanzoni mwa wiki hii, Ben Pol na mkewe huyo walionekana kwenye video wakiwa pamoja mtandaoni wakicheza kwa kukumbatiana huku mkewe akisema mumewe hakubadili dini. Wakati Anerlisa akisema hayo, Ben Pol anaonekana pembeni yake akicheka kwa furaha baada kauli hiyo ya mkewe.

 

Kufuatia mkanganyiko huo, mwanahabari wetu alimtafuta Shehe Alhad na kumueleza jinsi ambavyo ishu hiyo imeleta mkanganyiko ambapo aliuliza kama Ben Pol mwenyewe ndiye aliyesema hayo na alipoambiwa kuwa aliyesema ni mkewe huku Ben Pol mwenyewe akiwa pembeni akionekana kufurahia mkewe huyo anachoongea.

 

Shehe Alhadi alisema, kama aliyeongea ni mkewe na si Ben Pol mwenyewe, hawawezi kumpa hukumu yoyote mpaka aongee mwenyewe.

 

“Kama hakuongea mwenyewe hatuwezi kumhukumu kwa lolote labda angeongea mwenyewe na hapo angekuwa amerudi kwenye dini yake aliyotoka.

 

“Lakini hata hivyo, ninamuonya kuwa kufanya hivyo ni kosa kubwa, huwezi kuchezea dini ya watu, fanya masihara na mambo mengine, lakini siyo kuchezea dini ya watu,” alimalizia Shehe Alhad kwa kutoa onyo hilo.

 

Baadhi ya mastaa Bongo wamekuwa wakibadili dini kisha kurejea kwenye dini zao za awali, jambo linalowakwaza viongozi wao wa dini wakiwataka kuwa na msimamo thabiti kwenye masuala hayo ya kiimani.