Klabu ya Yanga imeuanza msimu wa 2020-21 vizuri tofauti na wengi walivyotarajia, mpaka sasa timu hiyo haijapoteza mchezo hata mmoja wa ligi na ipo nafasi ya pili kwenye msimamo na wanashikiria rekodi kadhaa hadi hivi sasa.

 

Yanga SC ndio timu pekee ambayo haijapoteza mchezo hata mmoja kwenye michezo ya ligi kuu Tanznaia bara VPL

 

Maandalizi ya kikosi cha timu ya wananchi hayakuwa yakuridhisha sana, ikiwemo timu kuchelewa kuingia kambini, usajili wa wachezaji ambao wengi wao walisajiliwa kipindi ambacho timu haikuwa na kocha mkuu lakini kubwa zaidi Yanga walimtangaza kocha mkuu ikiwa imebaki wiki moja kabla ya ligi kuanza.

 

Mfano, katika usajili wake, Yanga ilichukua nyota takribani 11 wapya Gifti Mauya, Bakari Mwamnyeto, Mustapha Yassin, Kibwana Shomari, Waziri Jr, Farid Mussa, Tonombe Mukoko, Tuisila Kisinda, Carlihos, michael Sarpong, na Yacouba Sogne.

 

Huo ni usajili ambao wengi walitegemea ingewachukua muda mrefu kupata muunganiko, na ni kweli chini ya Zlatko Krmpotic, Yanga ilishinda mechi 4 na sare moja katika mechi 5 za VPL, lakini kelele nyingi zilikua dhidi ya kikosi hicho ni kucheza soka gwaride, lisilo na ladha.

 

Soka Gwaride, Makande, lilipelekea Yanga wamfute kazi Zlatko, lakini bado waliendelea kusaka njia mbadala ya kubadili aina ya soka lao, huku wakiyasaka matokeo ambayo wameendelea kuyapata kiasi cha kuzua hovu kwa washindani wao wa karibu Simba na hata Azam.

 

Mpaka sasa Yanga wamefanya maajabu na hebu zipokee baadhi ya rekodi ambazo mpaka sasa Yanga imeziweka kwenye michezo ya ligi kuu Tanzania bara VPL.

 

Mosi ni kwamba Yanga ndio timu pekee ambayo haijapoteza mchezo hata mmoja kwenye ligi kuu Tanzania bara msimu huu, timu hiyo ya wananchi imecheza michezo 8 ya ligi imeshinda michezo 7 na wamapata sare kwenye mchezo 1 wakiwa na alama 22 wapo nafasi ya 2.


Kikosi hicho cha mabingwa wa kihistoria Tanzania bara kimeshinda michezo 7 ya ligi mfululizo ni rekodi na ndio timu iliyoshinda michezo mingi mfululizo sawa na Azam FC timu nyingine iliyofanya hivyo msimu huu.


Kikosi cha Yanga kimeshinda michezo yote 4 ya ugenini, na ndio timu iliyokusanya alama nyingi ugenini msimu huu alama 12.


Katika michezo 8 ya ligi kuu ambayo ni sawa na dakika 720 kikosi cha Yanga kimeruhusu magoli 2 tu, ikiwa ndio timu iliyoruhusu mabao machache mpaka sasa.


Yanga ni timu ya 4 kwenye orodha ya timu zilizofunga magoli mengi mpaka sasa kwenye VPL, kikosi hicho chini ya kocha Cedric Kaze kimefunga magoli 11 kwenye michezo 8 sawa na wastani wa bao 1.375 kwa mchezo.

 

Kikosi cha Simba ndicho kinachoongoza kwa kupachika mabao ambapo kimefunga magoli 19, Azam FC magoli 15, wakati KMC ina magoli 13.


Yanga pamoja na Azam ndio timu pekee ambazo hazijapoteza mchezo katika katika viwanja vyao vya nyumbani.

 

Katika michezo 4 ya nyumbani, Yanga imeshinda michezo 3 na sare mchezo 1, wakati Azam FC imeshinda michezo 4 na imetoka sare mchezo 1 kwenye michezo 5 iliyocheza nyumbani.