Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe. Aboubakar Kunenge amezindua kampeni ijulikanayo Kama “Usipime Nguvu ya Maji” inayolenga kudhibiti athari zitokanazo na Mafuriko yanayosababishwa na mvua.

RC Kunenge amesema tafiti zinaonyesha 73.6% ya vifo vinavyosababishwa na Mafuriko hutokana na watu kulazimisha kuvuka kwenye mito ya Maji inayopitisha maji huku 26.4% ya vifo hutokana na sababu za kawaida.

Aidha RC Kunenge amesema kampeni hiyo itahusisha utoaji elimu kwa wananchi wote wa jiji hilo wakiwemo wanafunzi, wafanyabiashara, watumiaji wa vyombo vya usafiri, watembea kwa miguu na Walemavu kwa njia ya vipeperushi na video clip zitakazokuwa zikionyeshwa kwenye Runinga, Blog, mitandao ya kijamii na mikutano.

Pamoja na hayo RC Kunenge ametoa wito kwa Wakazi wa mabondeni na waishio kwenye maeneo hatarishi kuchukuwa tahadhari mapema ili kukabiliana na athari za Mafuriko.

Hata hivyo amesema Serikali inaendelea kuboresha miundombinu ya mito, mitaro, madaraja na barabara ili kuhakishisha maji ya mvua yanapita Katika sehemu stahiki.

 

The post RC Kunenge azindua kampeni ya ‘Usipime Nguvu ya Maji’ ya kusaidia watu kwenye mafuriko DSM (+Video) appeared first on Bongo5.com.