TAARIFA kutoka Azam FC inaarifu kuwa mshambuliaji wao, Prince Dube, aliyeumia jana Novemba 25, kwenye mchezo dhidi ya Yanga, atasafirishwa kwenda Afrika Kusini Jumapili ya Novemba 29, kwa ajili ya matibabu zaidi baada ya kuvunjika mkono.


Dube alitolewa nje dakika ya 25 na nafasi yake kuchukuliwa na Richard Djodi baada ya majeraha hayo.

 

Taarifa hiyo inasema:

“Mshambuliaji wetu, Prince Dube, ambaye aliumia kwenye mchezo wetu dhidi ya Yanga jana Novemba 25, anatarajiwa kwenda Afrika Kusini kwa matibabu zaidi.

 

Dube raia wa Zimbabwe, aliumia dakika ya 15 kwa kuvunjika mfupa wa mbele wa mkono wake wa kushoto unaoitwa Ulnar. Huu ni mfupa unaoanzia kwenye kiwiko na kushuka hadi kwenye kidole cha mwisho.

 

Ataondoka nchini Jumapili ya Novemba 29 kwa ndege ya Shirika la Kenya Airways (KQ). Atatibiwa kwenye Hospitali ya Vincent Pallotti iliyopo Cape Town, chini ya daktari bingwa wa mifupa, Robert Nicolas.

 

Azam FC tumekuwa tukiitumia hospitali hii kutibia wachezaji wetu tangu mwaka 2011. Tunampa pole na kumtakia matibabu mema na kupona haraka, Prince Dube.